Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema mwenendo wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi unatoa taswira ya ushindi na kukubalika kwa Chama hicho na Watanzania.Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Dkt. Asha Rose Migiro, aliyefika Ikulu leo tarehe 08 Septemba 2025 kuonana naye baada ya kuteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo.

Rais Dkt. Mwinyi amempongeza kwa uteuzi huo wa kuwa Mtendaji Mkuu wa CCM Taifa na kueleza kuwa ana matumaini makubwa kutokana na uwezo wake.Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kufarijika na mwenendo wa Kampeni za CCM zinazoendelea katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, hali inayoashiria kukubalika kwa Chama hicho na ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Dkt. Mwinyi amemtakia mafanikio Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea wa CCM Taifa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.Vilevile, ameishukuru CCM Makao Makuu kwa msaada wake kwa CCM Zanzibar kuelekea uzinduzi wa Kampeni tarehe 13 Septemba 2025 Zanzibar.

Naye Katibu Mkuu, Dkt. Asha Rose Migiro, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kumuamini na ameahidi kushirikiana na CCM Zanzibar katika utekelezaji wa majukumu yake pamoja na kufanya kazi bega kwa bega wakati wa Kampeni.