Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amemshukuru Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Giuseppe Sean Coppola, kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya Zanzibar na Italia, hususan katika sekta ya utalii na utamaduni.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Balozi huyo Ikulu Zanzibar, akiwa na Balozi Mdogo wa Heshima wa Italia Zanzibar, Stephano Totisco.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuongezeka kwa safari za Shirika la Ndege la Italia (NEOS) hadi kufikia tano kuanzia Juni 2026, zitakazounganisha Zanzibar na miji ya Bari na Catania, kutaimarisha zaidi sekta ya utalii.
Aidha, ameeleza kuwa Zanzibar ipo tayari kuwa mwenyeji wa tamasha la muziki kutoka Italia litakalofanyika Ngome Kongwe, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kitamaduni.
Kwa upande wake, Balozi Coppola amepongeza maendeleo ya Zanzibar hususan katika miundombinu na pia kueleza kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kupitia Jukwaa la Biashara la EU–Tanzania, litakalolenga kilimo-biashara na mageuzi ya kidijitali linalotarajiwa kufanyika mwakani.
