Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi ulinzi wa uhakika siku ya uchaguzi na kuwataka kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kidemokrasia.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 25 Oktoba 2025, alipohudhuria Maombi ya Amani ya Kitaifa pamoja na kuuombea Uchaguzi Mkuu, yaliyoandaliwa na Umoja wa Makanisa Zanzibar katika Uwanja wa Michezo wa Kizimbani Dole, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Dkt. Mwinyi amesema Serikali zote mbili zimejiandaa kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura anapata fursa ya kutekeleza haki yake ya msingi ya kikatiba ya kuchagua viongozi.Aidha, ameeleza kuwa amani, muungano na mshikamano ni tunu za taifa ambazo Chama Cha Mapinduzi kimeahidi kuzilinda kwa maslahi ya wananchi wote bila kujali asili ya mtu au dini anayoabudu.

Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali zote mbili zimeondoa aina zote za ubaguzi ikiwemo ubaguzi wa dini, na kwamba itaendelea kudumisha sera hiyo ili kutoa uhuru wa kuabudu kwa waumini wa imani zote.Rais Dkt. Mwinyi ameushukuru Umoja wa Makanisa kwa kuandaa maombi hayo, aliyoyaelezea kuwa na umuhimu mkubwa hususan kipindi hiki cha kampeni na kuelekea siku ya uchaguzi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema taasisi za kidini zina wajibu mkubwa wa kuwaandaa waumini kuwa raia wema na kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hizo wakati wote.Dkt. Mwinyi ameuhakikishia Umoja huo wa Makanisa ushirikiano zaidi katika awamu ijayo, endapo wananchi watakipa ridhaa Chama Cha Mapinduzi kuiongoza tena Zanzibar, na kuzipongeza taasisi za kidini kwa misaada ya kijamii wanayotoa katika sekta za elimu, afya na maji kwa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia waumini wa Kikristo kuwa Serikali ipo tayari kuzifanyia kazi changamoto zote wanazokabiliana nazo hivi sasa pamoja na zile zitakazojitokeza baadaye.Mwenyekiti na Mratibu wa maombi hayo, Askofu Dickson Kaganga, ameahidi kwa niaba ya Umoja wa Makanisa Zanzibar kuendelea kuiombea nchi amani, umoja na mshikamano, ili lengo la kuwa na amani ya kudumu litimie, pamoja na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.