Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Michezo ya Majeshi Tanzania ni kielelezo cha ushirikiano na umoja wa kitaifa wa vyombo vya ulinzi nchini.Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 06 Septemba 2025, alipofungua Michezo ya Majeshi inayoratibiwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA), katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Mao Tse Tung, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameeleza kuwa michezo hiyo pia ni fursa muhimu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya michezo na kuviweka vyombo vya ulinzi karibu zaidi na wananchi.Rais Mwinyi amesema michezo ni daraja muhimu la kuunganisha vyombo vya ulinzi kuwa na mshikamano, hatua inayothibitisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi.

Aidha, amebainisha kuwa mwamko wa Watanzania kupenda michezo unazidi kukua siku hadi siku na unachangia kuimarisha afya za wananchi, nidhamu, mshikamano wa kijamii, ukuaji wa uchumi, pamoja na uvumilivu, utu na kuheshimu sheria.Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kujenga viwanja vya kisasa vinavyokidhi hadhi ya kimataifa na vigezo vinavyotambuliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) pamoja na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Vilevile, amesema malengo ya Serikali ni kuhakikisha michezo inafungua fursa za kiuchumi, kuimarisha ushirikiano, kukuza utalii na kuongeza ustawi wa jamii.Rais Mwinyi amesisitiza kuwa vyombo vya ulinzi vina mchango mkubwa katika michezo ya majeshi ambayo imekuwa chimbuko la wanamichezo mahiri wa Tanzania.

Aidha, ametoa rai kwa washiriki wa Michezo ya Majeshi Tanzania 2025 kuzingatia malengo ya michezo hiyo ya mshikamano na umoja wa wanamichezo, huku akiwapongeza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendeleza michezo hiyo kwa mafanikio.

Michezo hiyo iliyoanzishwa mwaka 1977, mwaka huu imeshirikisha kanda saba za JKT, Ngome, SMZ, Uhamiaji, Magereza, Zimamoto na Polisi.