Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha vijana kujifunza zaidi kuhusu astronomia, sayansi ya anga na teknolojia, ili waweze kutumia fursa zinazojitokeza katika sekta hizo kwa maendeleo ya Zanzibar. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 21 Septemba 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na uongozi wa Zanzibar Astronomy Space Society (ZASS), unaojihusisha na astronomia na sayansi ya anga Zanzibar.
Amesema elimu ya astronomia, sayansi na teknolojia ni muhimu katika kuwaandaa vijana kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia, kufanya tafiti, kuibua ubunifu na kutumia teknolojia za kisasa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo. Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza ZASS kwa juhudi za kuhamasisha astronomia na sayansi ya anga, hususan kwa vijana, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za elimu na wadau wa sayansi na teknolojia.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhiwa picha mbalimbali za astronomia zilizopigwa kutoka Zanzibar na ZASS, zikionesha maumbo na mandhari mbalimbali ya anga.
Naye Msemaji wa ZASS, Abuubakar Harith, amesema matumizi ya satelaiti yanaweza kusaidia katika tafiti na upatikanaji wa taarifa muhimu kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya Zanzibar, ikiwemo taarifa zinazohusu bahari, mazingira na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani.
