Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu, maslahi na mazingira ya kazi ya walimu ili kuwaongezea ari na motisha katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Akihutubia katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani, yaliyofanyika katika Viwanja vya Polisi Ziwani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa walimu katika maendeleo ya taifa na malezi ya vijana kielimu.
Ameeleza kuwa walimu ni fahari ya familia, taifa na jamii kwa ujumla, na ni daraja la kuifikisha jamii kwenye maarifa. Kwa msingi huo, Serikali imeiweka sekta ya elimu miongoni mwa sekta za kipaumbele kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta nyingine zote.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia walimu kuwa Serikali itaendelea kutoa ajira mpya kwa walimu kila mwaka, sambamba na kuboresha maslahi yao ikiwemo posho za kufundishia, ili kuongeza motisha na ari ya kazi.Aidha, Serikali imetenga fedha maalum kwa shule zote nchini kwa ajili ya mahitaji madogo madogo kama vile matengenezo na vifaa vya kufundishia.
Vilevile, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itazingatia ajira zaidi kwa walimu wa sayansi, TEHAMA, na biashara, na itaandaa posho maalum kwa walimu wanaofundisha shule tengefu na wale wanaowahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Ameongeza kuwa Serikali itajenga nyumba za maafisa ukaguzi wa elimu katika kila mkoa, kurasimisha elimu ya maandalizi, pamoja na ujenzi wa shule za maandalizi na utoaji wa posho za dhamana kwa walimu wenye dhamana, kwa mujibu wa sheria.
Halikadhalika, Rais Mwinyi ameahidi kulifanyia kazi ombi la walimu la kupatiwa mabasi maalum kwa usafiri wa kwenda na kurudi kazini, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaandalia mazingira bora ya kazi walimu nchini.“Ualimu ndio msingi wa maendeleo ya kila sekta. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuwatia moyo walimu wetu ili kuhakikisha tunapata elimu bora na mafanikio endelevu,” alisema Rais Dkt. Mwinyi.
Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 05 Oktoba, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Walimu Wetu, Fahari Yetu.”