Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kufarijika na juhudi pamoja na kazi nzuri za kuimarisha Dini ya Kiislamu zinazotekelezwa na Al Madrasat Swifat Nabawiyatil Karimah (Msolopa) ya Kilimani.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 15 Agosti 2025, alipokutana na uongozi wa chuo hicho uliofika Ikulu kuonana naye.Ameeleza kuwa kazi ya kuwafundisha vijana na watoto elimu ya dini inayofanywa na chuo hicho ni nyenzo muhimu ya kujenga jamii bora, na amesisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa jitihada hizo.
Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi ameahidi kushirikiana na kuunga mkono malengo ya chuo hicho, ikiwemo mradi wa ujenzi wa skuli itakayoweza kuchukua wanafunzi wengi zaidi, pamoja na kuwatafutia wafadhili.
Vilevile, Dkt. Mwinyi ameridhia ombi la uongozi huo la kupatiwa nafasi tatu za Hijja kwa walimu waandamizi wa chuo hicho, na kushiriki katika dua maalum ya kuwaombea viongozi wakuu na Taifa kwa ujumla, itakayofanyika tarehe 12 Septemba 2025.
Al Madrasat Swifat Nabawiyatil Karimah imeandaa Wiki ya Maadhimisho ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, itakayohusisha shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira, dua kwa viongozi na Taifa, kuzuru makaburi ya waasisi, kutembelea masheikh, uchangiaji wa damu na usomaji wa Maulid.