RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia masuala ya Mazingira (UN Environment) Mheshimiwa Joyce Msuya katika ukumbi wa Intercontinenatl Mjini Nairobi, na kulishukuru shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na na kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,hasa katika utekekelzaji wa miradi mbali mbali inayohusu mazingira na kuwajengea uwezo watendaji.
Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais alisema kwamba suala la mazingira lina umuhimu wa pekee katika nchi za visiwa katika wakati huu ambapo, dunia inakabiliwa na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na athari mbali mbali za kimazingira zinazosababishwa na shughuli za binaadam.
Mheshimiwa Rais, alieleza hivi sasa ni vyema ushirikiano uliopo baina ya shirika hilo ukazidi kuimarishwa ili kuweza kuisaidia Zanzibar katika utekelezaji mpango na miradi ya kutafuta na kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia.
Dk.Shein alisema kwamba Zanzibar bado haina wataalamu wa kutosha katika kuendeleza na kusimami sekta ya mafuta na gesi na Nyanja mbali mbali zinazogusa sekta hiyo, wakiwemo wataalamu wa mazingira.
Kwa hivyo, itakuwa ni vyema ikiwa Shirika hilo Iitasaidia Zanzibar katika kuandaa miongozo, sera na sheria muhimu zinahusu mazingira ili kuweza kuepuka athari za kimazingira zinazoambatana na sekta hiyo.
Katika kikao hicho,Dk.Shein alisema kwamba Zanzibar imejifunza mambo mengi kutoka katika nchi ambao hazikulipa umuhimu suala la mazingira wakati zilipoingia katika sekta ya mafuta na gesi.
Vile vile, alieleza kwamba itakuwa ni vyema ikiwa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linashughulikia masuala ya Mazingira litafikiria na kuangalia uwezekano wa kufanyakazi kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Programu ya pamoja inayojumuisha taasisi mbali mbali za Umoja wa Mataifa zilizopo Zanzibar ambayo aliizindua rasmi mwezi Agosti, mwaka huu 2018.
Alifahamisha kwamba, kupitia progarmu hiyo taasisi hizo zimekuwa zikifanyakazi na Serikali katika masuala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla, ikiwemo sekta ya afya, elimu, kujengea uwezo wafanyakazi, uwezeshaji na mapambano dhidi ya unyanyasaji na udhalishaji wa watoto.
Aidha Dk.Shein alimpongeza kiongozi huyo Kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo mkubwa katika ngazi taasisi ya Kimataifa na kusema kwamba uteuzi aliopata umezingatia uwezo na uzoefu alionao.
Kwa upande wake, Naibu Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia masuala ya Mazingira (UN Environment) Mheshimiwa Joyce Msuya alimshukuru mhe Rais Dk. Shein kwa kutenga muda maalum wa kukutana nae akiwa hapa Nairobi na kusema shirika lake litatoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha Zanzibar inafikia malengo yake iliyojiwekea katika suala la Mazingira.
Vilevile alielezea kuwa shirika hilo litaisaidia Zanzibar katika kuwajengea uwezo watendaji katika sekta ya Mazingira hasa wakati huu ambao Zanzibar imeingia katika uchumi wa sekta ya gesi asilia.