RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amehimiza ushirikiano bana ya taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, ndogo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja alipohudhuria hafla ya kuapishwa Mawaziri, Manaibu mawaziri, Katibu na Manaibu katibu wakuu na Mabalozi mbalimbali walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Dk. Mwinyi, aliwaeleza viongozi hao kwa waliopo kwenye Taasisi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi nyengine kuendeleza utamaduni wa ushirikiano na uhusiano mwema kwa taasisi hizo ili kuudumisha vema Muungano wa Tanzania.Aidha, aliwahakikishia ushirikiano viongozi hao baina yao na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwahidi kuuendeleza ushirikiano huo hata kwa taasisi zisizo za Muungano.
“Kwa taasisi zote za Muungano na zisizokuwa za Muungano, nakuhakikishieni kuendeleza utamaduni huu wa kuudumisha ushirikiano wetu kwa maslahi mapana ya Taifa letu, kuna taasisi nyengine sio za Muungano hapa Zanzibar lakini zimekua imara kuwajengea uwezo wenzao, nazipongeza sana” alieleza Rais Dk. Mwinyi.Hata, hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi walioapishwa kwa uteuzi wa nafasi zao.
Walioapishwa ni pamoja na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Mashaka Biteko, Mawaziri wanne, Naibu Mawaziri watano, Makatibu wakuu Watatu, Naibu Makatibu wakuu watatu pamoja na Mawaziri na Makatibu wakuu waliobadilishwa wizara zao.Hii ni mara ya Kwanza kwa Ikulu ndogo ya Zanzibar, Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja kuapishwa viongozi wakuu na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.