RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Serikali imejidhatiti kuzifikisha huduma za umeme katika maeneo yote wanayoishi wananchi kwa kutambua kuwa huduma hizo zinaenda sambamba na maendeleo ya dunia na siyo anasa kama ilivyokuwa hapo zamani.Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kuzindua umeme katika kisiwa cha Fundo kilichopo Jimbo la Gando, Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kutimiza miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Rais Dk. Shein alisema kuwa ukosefu wa huduma hizo unadumaza juhudi za wananchi katika kujitafutia maendeleo kwani umeme ni msingi wa maendeleo.Hivyo, Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa wananchi wa kisiwa hicho kuongeza kasi, ari na hamasa ya kutafuta maendeleo hasa kwa kujishughulisha na miradi ambayo mwanzo walishindwa kuifanya kwa kukosekana nishati hiyo. “Ni jambo la faraja kuona kwamba tumepiga hatua kubwa kufikisha huduma muhimu katika visiwa vidogo vidogo na vijiji vilivyo katika maeneo ya mbali kwani lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi wa Zanzibar popote alipo anapata huduma za umeme, afya, elimu, maji safi na salama na huduma nyenginezo”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa viongozi wote wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na Shirika la Umeme (ZECO) na Bodi yake kwa kuwa wepesi wa kutekeleza maagizo yake kwa kusimamia vyema Ilani ya CCM ya Uchaguzi kwa kipindi kilichomalizika na kilichopo hivi sasa cha 2015-2020.