Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na uongozi wa LIAONING FANGDA GROUP OF COMPANIES kutoka China, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Ao Xinhua, waliomtembelea Ikulu leo, tarehe 26 Machi 2026.

Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza kampuni hiyo kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na Zanzibar katika sekta mbalimbali za uwekezaji, na amewahakikishia ushirikiano wa kiwango cha juu.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar ina mipango endelevu ya kuimarisha sekta ya usafiri wa anga, kutokana na nafasi yake kama kitovu cha utalii, na kubainisha kuwa bado zipo fursa nyingi kwa wawekezaji kushirikiana na Zanzibar kuwekeza katika sekta hiyo.

Wakati huo huo Rais Dkt. Mwinyi amekutana na uongozi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Ndg. Khamis Juma Khamis.

Ujumbe huo uliambatana na wataalamu wa masuala ya teknolojia ya mifumo ya kidijitali kutoka Taasisi ya Deutsche Gesellschaft für Internationale Zusammenarbeit (GIZ) ya Ujerumani, inayoshirikiana na BPRA Zanzibar katika kuimarisha na kufanya mageuzi ya mifumo ya usajili pamoja na utoaji wa huduma za kidijitali.