Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia wavuvi, wachuuzi na wajasiriamali ili kuongeza kipato chao.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 30 Septemba 2025 alipokutana na wavuvi, wachuuzi wa samaki na wajasiriamali wa Diko na Soko la Samaki la Malindi, wakati akiendelea na kampeni zake na kuzungumza na makundi mbalimbali.
Kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo, Dkt. Mwinyi amesema kuwa utaratibu mzuri wa usimamizi wa masoko utaandaliwa ili kumaliza changamoto zinazowakabili katika maeneo wanayofanyia shughuli zao.
Aidha, amewahakikishia upatikanaji wa mikopo kwa wale ambao hawajapata katika awamu ya kwanza ya utoaji wa mikopo, na ameahidi ongezeko maradufu la fedha za mikopo kutoka shilingi bilioni 96 zilizotolewa awali.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kujenga madiko na masoko ya samaki pamoja na maeneo bora ya wajasiriamali Unguja na Pemba, ili kuwe na mazingira bora na vifaa kwa wavuvi, ikiwemo boti za kisasa za uvuvi na vitendea kazi vya kisasa vitakavyowawezesha kuvua bahari kuu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyaomba makundi hayo kumchagua tena kuiongoza Zanzibar ili atekeleze ahadi anazozitoa sasa na kuleta maendeleo zaidi.