RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwachukulia hatua kali wawekezaji au waajiri wote wanaokwenda kinyume na sheria za Serikali. Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana mashirikiano ya Sekta binafsi na kusisitiza kuwa wawekezaji au waajiri wanaodharau sheria au maslahi ya wananchi hawatovumiliwa hata kidogo. Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ukumbi mdogo wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo Zanzibar inaungana na nchi nyengine duniani katika maadhimisho hayo ambapo mapema Dk. Shein alipokea maandamano ya wafanyakazi
Rais Dk. Shein alisema kuwa inasikitisha kwamba kuna baadhi ya wawekezaji na waajiri ambao walitaka kuzikwamisha juhudi za Serikali ambapo walijaribu kuupinga uwamuzi huo wa Serikali. Hata hivyo, Dk. Shein alisema kuwa amefurahi kuona kwamba hivi sasa wananchi wengi wanaofanya kazi katika sekta binafsi, wameanza kufaidika na kiwango cha mshahara kilichotangazwa na kueleza kwa wale waliokuwa hawamudu imewawekea utaratibu na kanuni maalum. Katika maadhimisho hayo ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Dk. Shein alieleza kuwa yeye ni kiongozi ambaye amekuwa akitaka wafanyakazi wawe na mishahara mizuri kila pale hali inaporuhusu na kueleza kuwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hakuna mfanyakazi aliyekatwa mshahara na kiliopo ni kupangwa kwa wafanyakazi wote wa sekta ya umma na mashirika ya serikali mishahara yao ilingane. Aliongeza kuwa kutokana na juhudi za serikali na wafanyakazi wa Zanzibar uchumi wake umeimarika kutoka asilimia 6.8 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 7.5 na pato la mtu binafsi limeongezeka kutoka TZS 1,800,000 hadi TZS 2,000,000 mwaka 2017 na mfumko wa bei ulipungua kutoka 6.7 mwaka 2016 na kufikia 5.6 mwaka 2017. Aidha, kupungua kwa utegemezi wa bajeti kutoka asilimia 30.2 katika mwaka 2010/2011 hadi kufikia asilimia 7.3 mwaka 2017/2018.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kupima afya kwa wafanyakazi wote na kuwashajiisha kufanya mazoezi kupitia vikundi mbali mbali vilivyoanishwa ili kuwakinga na maradhi huku akisisitiza kuwa UKIMWI bado upo hivyo tahadhari bado zinahitajika. Kutokana na wanawake wengi hivi sasa kukumbwa na vifo vinavyotokana na ongezeko la maradhi ya Saratani ya Shingo ya Kizazi, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kumuunga mkono Mama Shein kwa kuzindua kampeni hiyo kwa upande wa Zanzibar na Makamo wa Rais Mama Samia aliyezindua kwa upande wa Tanzania Bara mnamo tarehe 10 mwezi uliopita. Kadhalika, Dk. Shein aliwahimiza wafanyakazi kuunga mkono juhudi za Serikali na jamii katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia jambo ambalo limekuwa ni tatizo kubwa nchini hasa katika miaka ya hivi karibuni. Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kuweka mazingira bora yenye kuhakikisha kwamba vyama vya wafanyakazi vinaundwa, vinanawiri na vinatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria. “Nakusisitizeni viongozi wa vyama vya Wafanyakazi muendelee kushirikiana na Serikali katika kuimarisha uwajibikaji, maadili pamoja na kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma”,alisema Dk. Shein. Alieleza kuwa rushwa ipo na ushahidi upo na wafanyakazi wapo wanaochukua rushwa na Serikali inaendelea kuwashughulikia.
Aidha, kuhusu tatizo la ajira kama ilivyo katika mataifa mbalimbali duniani, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa vikundi mbali mbali vya wajasiriamali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji. Alisisitiza kwamba katika suala zima la ajira hakuna ubaguzi wa ajira na wala hawaajiriwi watu kwa kisingizio cha wale wanaotoka katika chama tawala. Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwaajiri vijana katika sekta mbali mbali kwa kadri nafasi zinavyopatikana huku akieleza kuvutiwa na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Njia Pekee ya Kukuza Uzalishaji na Kuimarisha Huduma, ni Kujadiliana na kujali Ushirikishwaji”, alisema Dk. Shein. Dk. Shein pia, aliwataka wananchi waendelee kufanya kazi na kueleza kuwa uongozi wa kidemokrasia hupatikana kwa uchaguzi mkuu na hivyo kwa hivi sasa hakuna tena uchaguzi mpaka 2020. Aidha, Dk. Shein alisikitishwa na wale wafanyakazi wote wanaofanya vituko makazini ikiwa ni pamoja na kufanya ubadhirifu wa mali ya umma na kuahidi kuwa ataendelea kuwatumbua wale wote wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi. Pamoja na hayo aliwasisitiza wafanyakazi na wananchi kuzingatia sana umuhimu wa kuishi kwa amani na utulivu kwani ndio stahili ya nchi yetu hatua ambayo imepelekea maendeleo makubwa kwani fujo hazisaidiii kwani serikiali haipambani na wananchi wake bali inawaongoza wananchi wake.
Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico alitoa pongezi kwa Shirika la ILO na kuvipongeza vyama vya ZANEMA na ZATUC kwa kutekeleza majukumu yao na kuahidi kushirikiana nao. Mapema Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani Antony Rukuzibwa alieleza suala la majadiliano ya pamoja yamechukua ujumbe mkubwa katika maadhimisho ya Mei Mosi ya mwaka huu, na kupongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kufanya majadiliano na kuvishirikisha vyema vyama vya wafanyakazi katika masuala tofauti. Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA) Salah Salim Salah alieleza haja kwa Wizara ya Elimu kushirikiana na Jumuiya hiyo ili waweze kutoa michango yao ili kuwafanya vijana waweze kupata kujiajiri wenyewe. Katibu Mkuu wa ZATUC Khamis Mwinyi Mohamad akisoma risala ya wafanyakazi wa Zanzibar alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuwajali wafanyakazi kwa kuengeza mishahara mara nne, kuwapa wazee pencheni, kuongeza na mengineyo huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono.