Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imejipanga kufanya kazi ya ziada katika Awamu Ijayo ili kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali.

Akizungumza na makundi hayo leo tarehe 30 Septemba 2025 katika Soko la Kibanda Maiti, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi alisema tayari michoro ya Soko la Kisasa la Kibanda Maiti imekamilika na fedha za kutosha zimetengwa ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali ijayo itaimarisha upatikanaji wa mikopo isiyo na riba kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, huku wale wanaoonyesha rekodi nzuri ya urejeshaji mikopo wakiongezewa fursa zaidi.

Dkt. Mwinyi aliwaomba wananchi kuendelea kuamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumchagua yeye pamoja na wagombea wa chama hicho katika ngazi zote, ili kuweza kutekeleza kwa mafanikio ahadi zinazotolewa sasa.

Vilevile, amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuhakikisha CCM kinapata ushindi wa kishindo.