Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Afya wakati Wizara hiyo ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango
Kazi wa Mwaka 2016/2017, 2017/2018 na Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba, mwaka 2017.

Dk. Shein, alifurahi baada ya kupata taarifa kutoka kwa uongozi wa Wizara hiyo kwamba hali ya upatikanaji wa dawa za maradhi mbali mbali Zanzibar iko vizuri na kusisitiza juu ya umakini na usimamizi mzuri wa utoaji wa dawa hizo ili kulinda afya za wananchi na kuepuka ubadhirifu katika utoaji wake.

Hivyo aliwaeleza viongozi hao, haja ya kuwajuilisha na kuwaelimisha wananchi juu ya uwepo wa aina mbali mbali za dawa na vigezo vinavyozingatiwa katika utoaji wake.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na wafanyakazi wote wa Wizara ya Afya na kueleza haja kwa Wizara hiyo kuendelea kusimamia vyema huduma za afya kwa wananchi pamoja na kuendelea kutoa elimu ya afya kwa jamii.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kuwaeleza wananchi kuwa lengo la Mapinduzi ya Januari 12, 1964 lipo pale pale katika kuwapa wananchi matibabu bure na pale panapotokea upungufu ndio hupaswa kuchangia.

Katika kikao hicho Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd nae alihudhuria ambapo Dk. Shein pia, alisifu hatua iliyofikiwa katika kujitolea
kutoa damu na kuwapongeza wananchi kwa jinsi wanavyojitokeza kwa wingi kutoa damu.

Aidha, alitilia mkazo katika kutoa mafunzo ya huduma za meno kwa kuzingatia kwamba hadi sasa Zanzibar wapo wataalamu wachache katika fani hiyo. Aidha,
alifahamisha kwamba itakuwa ni vyema ikiwa chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kitaanza kutoa mafunzo hayo pamoja na Wizara ya Afya kupeleka wanafunzi nje ya nchi kusomea fani hiyo.

Aidha. Aliutaka uongozi wa Wizara ya Afya kulilinda vizuri eneo la Binguni ambalo limetengwa maalum kwa ajili ya Ujenzi wa Hospitali ya kisasa na
kuwaagiza viongozi hao kuwa wepesi kuwachukuliaa hatua za kisheria watu wanaojitokeza kuvamia eneo hilo.

Nae Waziri wa Wizara ya Afya Mahmoud Thabit Kombo alieleza kuwa hali ya dawa katika hospitali za Unguja na Pemba inaendelea kuwa nzuri
na katika kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka 2017 Wizara imepokea dawa na vifaa tiba kutoka mfuko mkuu wa Serikali na Washirika wa Maendeleo.

Waziri Kombo alieleza kuwa miongozo, utaalamu na uzoefu na maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa Dk. Shein kwa Wizara hiyo yamekuwa chachu ya kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo.

Nao uongozi wa Wizara ya Afya ulieleza hatua wanazoendelea kuzichukua katika kupambana na maradhi ya Malaria na kueleza mikakati waliyoiweka katika kukabiliana na maradhi hayo hasa kwa baadhi ya Shehia katika Wilaya ya Magharibi A, Magharibi B, Wilaya ya Kati na Wilaya ya Micheweni Pemba.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa maambukizi ya maradhi ya Malaria hapa Zanzibar yapo chini ya asilimia 0.5 hali inayoonesha mafanikio makubwa yaliopatikana
katika kupambana na maradhi hayo.

Pia, uongozi huo ulieleza kuwa maradhi mbali mbali, yakiwemo kichocho, minyoo, homa ya matende yamepungua kwa kiasi kikubwa huku wakieleza mafanikio yaliopatikana katika upatikanaji wa damu, ambapo Wizara hiyo imeweza kukusanya zaidi ya kiwango kilichokadiriwa lakini changamoto iliopo ni katika matumizi.

Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa Wizara ya Afya katika kuimarisha nguvu kazi katika sekta hiyo, Wizara imeendelea kuwapatia mafunzo ya muda
mrefu wafanyakazi wake ambapo imewapeleka masomoni wafanyakazi 67 wa kada mbali mbali, wakiwemo madaktari wa usingizi, wauguzi, wataalamu wa mionzi, Clinical Audiology, matatizo ya kisaikolojia, ushauri nasaha na Dermotology.

Pia, uongozi huo ulieleza kuwa kuwepo kwa miundombinu imara na ya kutosha pamoja na vifaa vya kufanyia kazi ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo yameweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha kutoa huduma bora za afya.