Hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais Dk. Shein, ilifanyika hapo jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Zanzibar ambapo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nao walihudhuria.

Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Oman pamoja Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walihudhuria ambapo kwa upande wa Serikali ya Oman Waziri wa Mafuta na Gesi wa nchi hiyo Dk. Mohammed bin Hemed Al Ruhmi aliongoza ujumbe wa Oman.Taarab hiyo ilienda sambamba na chakula hicho maalum cha usiku kilichoandaliwa na Rais kwa ajili ya wageni hao na kuweza kutoa burudani murua ambayo iliweza kuwafurahisha
wageni pamoja na wenyeji wa hafla hiyo.

Waimbaji wa kikundi hicho cha Taifa cha taarab waliimba nyimbo mbali mbali za taarab zikiwemo zile za asili ambazo hadi hivi leo bado zinaendelea kupendwa kutokana na muziki na ala zake sambamba na ujumbe
uliomo kwenye nyimbo hizo.

Waimbaji mahiri kutoka katika kikundi hicho waliweza kutoa burudani safi ya nyimbo zao akiwemo Sabina Bint Hassan aliyoimba nyimbo isemayo ‘Kama yalivyonipata’ nyimbo iliyotungwa na Mzee Haji na kutiwa sauti na
Abass Machano.

Professa Mohammed Ilyas naye hakuwa nyuma katika kutoa burudani kwenye usiku huo maalum kwa kuimba nyimbo isemayo ’Nipepee’, ambapo naye Saada Nassor aliimba wimbo uitwao ‘Kibali’, wimbo uliotungwa na Chimbeni Kheir na kutiwa sauti na yeye mwenye Chimbeni Kheir ambaye hivi sasa ni Mshauri wa Rais katika masuala ya utamaduni, utalii na michezo.

Makame Faki na nyimbo yake ‘Tumependana wenyewe’ nyimbo iliyotungwa na Nasma Khamis na kutiwa sauti na yeye mwenyewe Makame Faki almaarufu Sauti ya Zege, nayo iliweza kukonga nyoyo za hadhira hiyo iliyofika
katika hafla hiyo sambamba na nyimbo ‘Nnae’ iliyoimbwa na Idd Suwed.

Makofi,hoihoi, nderemo na vigeregere vilisikika katika ukumbi huo pale wageni kutoka Serikali ya Oman walipoomba wimbo wa ‘Kama yalivyonipata’ uimbwe tena na bila ya ajizi Sabiha Bint Hassan na kikundi chake hicho cha Taifa uliirejea nyimbo hiyo.

Akitoa neno la shukurani katika hafla hiyo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Gavu alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano kati yake na Serikali ya Oman kwa mafanikio ya pande zote mbili.

Waziri Gavu aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itaendeleza uhusiano, ushirikiano pamoja na umoja uliopo kati yake na Oman huku akipongeza juhudi zinazochukuliwa kwa kila upande
katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.

Aidha, Waziri Gavu alieleza kuwa kuwepo kwa uhusiano na kukuza ushirikiano uliopo ni mbegu ya kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Oman na Zanzibar.