RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Jumuiya ya Fisabil llah Markaz kwa nia yao njema ya kumuombea dua na kuliombea dua taifa. Alisema, majukumu mazito waliyonayo viongozi wa nchi yanabeba dhima kumbwa kwa taifa na watu wake, hivyo wanahitaji kuombea dua kwa nia yakufanikisha vyema majukumu yao kwenye utendaji wao wa kila siku.
Al hajj Dk. Mwinyi, aliyasema hayo kwenye dua maalum ya kumuombea yeye na taifa kwa kipindi chote cha uongozi wake, dua hiyo imefanyika baada ya Ibada ya Sala ya Ijumaa, Masjid Mushawar, Mwembeshauri Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.Alisema, kuna wakati mambo yanakua magumu, kama kiongozi mkuu wa nchi, kila jambo linalotokea nchini linamuhusu na kumuwajibikia liwe zuri au baya na ufumbuzi wa magumu yote yanayotokea nchini ni kuomba dua, kila mara tuiombea nchi yetu na viongozi wake.
Akizungumzia athari za madhara ya dini na siasa yanapokosa uratibu mzuri nchini Al hajj Dk. Mwinyi alisema mara nyingi huwa chachu ya uvunjifu wa amani na mshikamano wa watu, hivyo ameishukuru Ofisi ya Mufti Zanzibar kwa uratibu mzuri wa masuala yote ya dini hali iliyochangia amani, ushirikiano, umoja na mshikamano uliuopo kwa wananchi wa Zanzibar.Al hajj Dk. Mwinyi pia alihimiza umuhimu kuiombea dua nchi na dunia kwa ujumla kwani mabaya yote yanayotokea kwenye mataifa makubwa huathiri dunia nzima kiuchumi na kijamii.
Alisema, vita vinavyopiganwa mataifa makubwa duniani pamoja na majanga ya ulimwengu yamesababisha mfumuko wa bei za bidhaa na chakula duniani kote hasa mafuta hali inayoleta taharuki na ugumu wa maisha na kupanda kwa gharama za Uchumi duniani kwa mataifa mengi kuathiriwa na hali hiyo.Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman alipongeza juhudi za vitendo anazozifanya Al hajj Dk. Mwinyi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo ya uongozi wake katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na kuendelea kuhimiza amani, utulivu na mshikamano kwa wananchi wote.
Mapema, akizungumza kwenye ibada hiyo, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume alimweleza Al Hajj Dk. Mwinyi kwamba Shughuli zote za dini zinazosimamiwa na Ofisi hiyo zimeimarika na kuendelea kwa ufanisi wa hali ya juu.
Naye, Khatibu wa ibada ya sala ya Ijumaa msikitini hapo, Shekh Abubakar amewahimiza waumini hao kukithirisha dua kwenye sijda zao kwani Mwenyezi Mungu (S.W) hujibu haraka dua za waja wake wanyenyekevu.Akitoa shukurani kwa Al Haj Dk. Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Fisabil llah Markaz, Amir Hafidh Jabu kwa msaada mkuwa anaoutoa kwa jumuiya hiyo, tokea kuingia madarakani ndani ya kipindi chote cha miaka mitatu ya uongozi wake.
Alisema, tokea kuingia madarakani Al Hajj Dk. Mwinyi amekua msaada mkubwa wa kuunganisha waumini wa Dini pamojana kutoa nguvu kubwa kwa jumuiya hiyo hali iliyoshajihisha kwa viongozi wengijne wa Serikali kuendelea kuiunga mkono jumuiya hiyo.