Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema mashindano ya Dunia ya Kuhifadhi Qur’aan yamekuwa kivutio na kitambulisho chengine muhimu cha kuitambulisha Zanzibar katika jukwaa la kimataifa. Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 14 Machi 2026, katika Mashindano ya Tatu ya Dunia ya Kuhifadhi Qur’aan yaliyofanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kushika muongozo wa Qur’aan ili kuwa na jamii iliyoongoka, sambamba na kushikamana na Sunnah za Mtume Muhammad (SAW) ili kuongozwa na kupata fadhila za Mwenyezi Mungu. Halikadhalika, amewasisitiza washiriki na washindi wa mashindano hayo kujifunza tabia njema, akieleza kuwa lengo la kuhifadhi Qur’aan si kupata vyeti pekee, bali ni kuishi kwa nidhamu na kukuza utamaduni wa Kiislamu katika maisha yao ya kila siku.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo kwa mafanikio kwa miaka mitatu mfululizo. Mashindano ya mwaka huu ya Dunia ya Kuhifadhi Qur’aan yameshirikisha washiriki kumi na moja (11) kutoka mataifa mbalimbali.
Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza alikuwa Abdulaaziz Ali Khamis kutoka Zanzibar aliyepata pointi 99.5 na kujishindia shilingi milioni 30. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Ibrahim Usman Ibrahim kutoka Nigeria aliyepata pointi 99 na kujishindia shilingi milioni 20, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Adan Ismail kutoka Marekani aliyepata pointi 98.5 na kujishindia shilingi milioni 10.
Vilevile, katika Mashindano hayo yalihusisha vipengele vya kuhifadhi Juzuu 30 za Qur’aan, usomaji wa Adhana pamoja na usomaji wa Qur’aan kwa mtindo wa Tashjih Tahakik.
Mashindano hayo yamehudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi, viongozi mbalimbali wa Serikali, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa dini, wanazuoni wa Qur’aan pamoja na wananchi na wageni kutoka mataifa mbalimbali.
