RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uongozi mpya wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufuatia kuteuliwa kwao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na viongozi hao waliofika kujitambulisha.

Dk. Mwinyi aliwasifu kwa kuteuliwa kwao na kueleza ni moja kati ya Wizara muhimu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoibeba nchi nje ya mipaka yake.
Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia ushirikiano wa kutosha uongozi huo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza Serikali inaridhirishwa na ushirikiano wa kiutendaji unaoupata kutoka kwa taasisi za Serikali za Jamhuri ya Mungano Tanzania haswa kwa taasisi za Muungano na sizizo za Muungano katika kuweka ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za Serikali zote mbili.

Uongozi mpya wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, uliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, Agosti 30 mwaka huu na baadae kuapishwa Septemba mosi mwaka huu, Ikulu ndogo Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja kufuatia kufanya mabadiliko madogo ya Baraza lake la Mawaziri.

Walioteuliwa ni Waziri wa Wizara hiyo, Januari Yussuf Makamba ambae awali alitokea Wizara ya Nishati na Balozi Dk. Kennedy Gastorn alieteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anaeshugulikia masuala ya Afrika Mashariki.