RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi jana usiku alijumuika na wananchi na viongozi mbalimbali wa chama na serikali kwenye taarabu rasmi ya maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo.Taarabu hiyo ilitumbuizwa na vikundi viwili tofauti kikiwemo kikundi cha sanaa cha taifa pamoja na kikundi cha “Island Morden taarabu, maarufu kama Wajelajela” ilikua maalumu kwa kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 pamoja na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani kipindi cha miaka miwili ya uongozi kwa kuiletea Zanzibar maendeleo makubwa.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa ndege, Zanzibar ulipambwa kwa vifijo na hoi hoi kutoka kwa wasanii wa vikundi hivyo, aliomudu vyema kukonga nyoyo za wananchi waliohudhuria kutokana na umahiri wao wa kucharaza ala pamoja kughani nyimbo mbali mbali, zilizotoa hamasa na kupamba usiku wa Mapinduzi mbele ya Rais Dk.  MwinyiWasanii nguli kutoka “Wajelajela” walifanikiwa kuitawala vyema hadhira iliyojumuika nao kwa kulidhibiti vizuri jukwaa kiasi cha kuwafanya watazamaji na wasikilizaji wao kushindwa kujizuia na kuibua vifijo na nderemo.

Miongoni mwa nyimbo zilizovuta hisia na kushangiliwa muda wote ni ile ya “Walisema hatuwezi nawaje kututizama” ulioimbwa na Ustadh Hafidh Abdulsalam, wimbo wa “Kweli nnaye” ulioghaniwa na Ustadh Iddi bin Suweid, wimbo wa “Kimeniasiri nini” ulioimbwa na msanii mahiri (Al – anisa, Husna kitoto)  na wimbo wa “Mbona watakereka sana” ulioimbwa na (Al – anisa, Sabah Salum).Nyimbo nyengine zilizoimbwa usiku huo ni pamoja na wimbo wa “Mapinduzi” ambao uliimbwa na wasanii wote walioburidisha hafla hiyo, wimbo wa “Mimi nae damdam” ulioghaniwa na Al-anisa, Rukia Ramadhan, “Ukewenza” uliimbwa na Al-anisa Amina Hamad na Ustadh Maliki Hamad, wimbo wa “Kama yalivyonipata” uliimbwa na (Al – Anisa, Sabina Hassan), “Hakika Nnakupenda” uliibwa na Profesa, mkongwe wa taarabu nnchini, Ustaadh Moh’d Iliyas, wimbo wa “Mkodombwe” ulitumuizwa na Al – anisa, Safia Yahya.

Naye, Ustadh Hassan Vocha akakonga nyoyo za washabiki wake kwa nyimbo za “Kupendwa na Rejea tena chuoni”, nyimbo za “Mnaminami Viumbe” na “Mbona Mtakereka sana” ambazo zilihaniwa na (Al-anisa, Sabah Salum).

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, na Michezo, Fatma Hamad Rajab alizungumza kwenye hafla hiyo na kueleza kwamba taarabu hiyo ya kihistoria ilikua maalum kwaajili ya kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa nchi ya ufunguzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Taarab hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, pamoja na viongozi wengine wa chama na Serikali