Media » News and Events

Dk.Mwinyi ameuhakikishia uongozi wa Aga Khan kuwa itaratibu sheria nzuri za kuwavutia wawekezaji.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi ameuhakikishia uongozi wa Taasisi ya Aga Khan kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane inaweka taratibu na sheria nzuri za kuwavutia wawekezaji.Rais Dk Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Ikuku Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Ujumbe wa Taasisi ya Aga Khan nchini Tanzania ukiongozwa na Amir Kurj, Mwakilisghi Mkaazi wa Taasisia ya Aga Khan akiwa amefuatana na Rais waJumuiya ya Ismailia pamoja na Mehiboob Chapsi Mjumbe wa Taasisi hiyo.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Hussein alisema kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inawawekeza mazingira mazuri wawekezaji wa ndanai na nje ya nchi ambao wanalengo la kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii, viwanda na nyenginezo.Alisisitiza kuwa kipaumbe cha Serikali ya Zanzibar Awamu ya Saba hivi sasa imelenga kuendesha na kukuza uchumi wa buluu kwa kuzitumia kikamilifu rasimali zinazohusiana na bahari, ikiwemo shughuli zinazohusu sekta ya utalii, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi na bahari kuu, ufugaji na usindikaji wa samaki, ukulima wa mwani na nyenginezo.

Hivyo, aliongeza kwamba jitihada hizo zinahitaji mikakati madhubuti ya kuhakikisha malengo yaliofikiwa na Serikali yanafikiwa na ndio maana Serikali imeamua kwa makusudi kuhakikisha inaweka mazingira bora kwa wawekezaji.Rais Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kuikaribisha Taasisi hiyo ambayo inahistoria ndefu katika kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii pamoja na huduma za kijamii kama vile elimu na afya.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Hussein Mwinyi aliipongeza Taasisi hiyo kwa kuekeza hapa nchini katika sekta ya utalii pamoja na kusaidia katika kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya ambapo hatua hizo zimeleta tija kwa wananchi wa Zanzibar.Aidha, Rais Dk. Hussein alisema kuwa Taasisi ya Aga Khan ina uzoefu mkubwa wa mashirkinao hapa Zanzibar hivyo Serikali itaendeleza uhusiano na ushirikiano huo wa muda mrefu kwa azma ya kuiletea maendeleo Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Hussein aliueleza ujumbe huo kwamba Serikali imeamua kwa makusudi kuwajengea uwezo na kuwasaidia wananchi wa ngazi ya chini hivyo, ni vyema miradi itakayobuniwa na Taasisi hiyo ikawalenga wananchi hao hapa Zanzibar.Wakati huo huo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alitoa shukurani na pongezi kwa kiongozi Mkuu wa Aga Khan duniani Mtukufu Karim Aga Khan ambaye pia ni kiongozi wa kiroho wa Madhehebu ya Kiislamu ya Shia Ismailia kwa kumtakia salamu za pongezi kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi Mkuu uliopita hapa nchini.

Rais Dk. Hussein alimpongeza Mtukufu Karim Aga Khan na kumuhakikishia kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar itaendeleza mashirikiano mazuri na ya muda mrefu yaliopo kati yake na Taasisi hiyo kwani inathamini na kutambua mchangio mkubwa uliotoa Taasisi hiyo katika sekta mbali mbali.

Mapema Mwakilishi Mkaazi wa Taasisi ya Aga Khan Amin Kurji alimpongeza rais Dk. Hussein Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kumuahidi kwamba Taasisi hiyo itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake.Kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwamba Taasisi ya Aga Khan imekuwa na mashirikiano na Zanzibar kwa muda mrefu na imekuwa ikiiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi mbalim mbali.

Aliongeza kuwa tokea kusainiwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduizi ya Zanzibar na Taasisi hiyo mnamo mwaka 1988 ambapo historia inaonesha kwamba babu yake Mtukufu Aga Khan alianzisha skuli ya mwanzo katika Afrika Mashariki ya wanawake hapa Zanzibar mnamo mwaka 1905.

Kiongozi huyo pia, alimueleza Rais Dk. Hussein miradi mbali mbali iliyoanzishwa na Taasisi hiyo hapa nchini ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar kwa kusaidia Mapngo Mkuu wake mnamo mwaka 1994 na baadae kuingia katika “Urithi wa Dunia” kupitia UNESCO.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo alieleza azma ya Taasisi hiyo kuendeleza kutoa huduma za kijamii kama ilivyokuwa ikifanya hapo siku za nyuma ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu ya dini na ile ya dunia sambamba na kutoa nafasi za masomo kwa elimu ya juu kwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) cha Dar-es Salaam, ambapo Taasisi hiyo imekuwa ikisaidia.

Pia, kiongozi huyo alieleza hatua mbali mbali mbali zilizochukuliwa na Taasisi hiyo katika kuimarisha Taasisi iliyokuwa ya Kiserikali (NGOs) mnamo mwaka 1999 huku akieleza jinsi Taasisi hiyo ilivyoshiriki katika kuimarisha utalii kwa kujenga hoteli ya Serena iliyopo ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, kuifanyia ukarabati mkubwa bistani ya Forodhani, kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la “Old Dispensary” pamoja na majengo mengine ya Mji Mkongwe.

Kiongozi huyo pia, alimkabidhi Rais Dk. Hussein Mwinyi salam za pongezi kutoka kwa kiongozi Mkuu wa Aga Khan duniani Mtukufu Karim Aga Khan zilizopomgeza Rais kwa ushindi mkubwa alioupata kufuatia uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2020