SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imemuhakikishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Watanzania wote walioko nchini China wako salama huku nchi hiyo ikiendelea kutafuta tiba ya kudumu ya virusi vya corona.
Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anaefanyia kazi zake hapa Zanzibar Xie Xiaowu aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Rais Dk. Shein, Ikulu Jijini Zanzibar ikiwa ni pamoja na kumpa taarifa ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona ulioanzia nchini China.
Katika maelezo yake Balozi Xie Xiaowu alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China inaendelea na juhudi zake katika kuhakikisha maradhi yanayosababishwa na virusi vya corona yanapatiwa tiba ya kudumu.
Balozi Xie Xiaowu alieleza kuwa Serikali ya China chini ya kiongozi wake Rais Xi Jinping inaendelea na juhudi zake na tayari imeanza kupata mafanikio katika kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya homa ya corona nchini humo na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na China.
Hivyo, Balozi Xie Xiaowu alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China inaendelea kupambana na maradhi hayo nchini humo na kumuhakikishia kuwa Watazania wote wanaoishi nchini humo wakiwemo wanafunzi wako salama.
Aliongeza kuwa kwa vile Jamhuri ya Watu wa China inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchi hiyo inaendelea kuwatunza na kuwapa huduma zote muhimu Watanzania waliopo nchini humo kama inavyofanya kwa wananchi wake.
Balozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa nchi yake inaendelea kuwapa uangalizi mkubwa Watanzania wote waliopo nchini China sambamba na kuhakikisha wanaishi kwa salama na amani hasa katika kipindi hichi cha mripuko wa ugonjwa huo.
Aidha, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya Afya ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kinga juu ya kusambaa kwa virusi vya corana.
Alisisitiza kuwa kwa vile Zanzibar ni visiwa ambavyo vimekuwa ni vivutio vya utalii hali ambayo inapelekea wageni kutoka mataifa mbali mbali kuja kuitembelea, hivyo, ipo haja ya kuwekwa mikakati maalum na kuchukua tahadhari kubwa katika kupambana maambukizi ya na virusi vya corona kutoka kwa wageni wote wanaoingia nchini.
Balozi huyo alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutuma salamu za pole na rambirambi kwa Rais Xi Jinping kufuatia China kukumbwa na ugonjwa huo uliopelekea vifo pamoja na wananchi kadhaa kuugua.
Wakati huo huo, Balozi Xie Xiuowu alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Benki ya Exim imeshakuwa tayari kutoa fedha kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa jengo la Abiria (Terminal III) la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.
Balozi huyo alimueleza Rais Dk Shein kuwa changamoto zilizokuwepo ambazo zilipelekea kuchelewesha kupatikana kwa fedha hizo kutoka Benki hiyo ya Exim tayari zimepatiwa ufumbuzi na wakati wowote fedha hizo zitatolewa kwa ajili ya kukamilisha taratibu za ujenzi kama ilivyopangwa hapo mwanzo.
Aidha, Balozi huyo alimuahidi Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha anachukua juhudi za makusudi za kuitaka Kampuni inayojenga uwanja huo kutoka nchini China inamaliza ujenzi wa jengo hilo kwa wakati uliopangwa na kwa kiwango kizuri kilichokusudiwa ili kukidhi haja ya kuhudumia ndege za ndani na za Kimataifa.
Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alitumia fursa hiyo kwa kutoa pole kwa janga hilo lililoikumba nchi hiyo na kueleza kuwa wananchi wa Zanzibar na Jamhuri yote ya Muungano wa Tanzania wako pamoja na ndugu zao wa China katika kuwaombea.
Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar itaendelea kushirikiana na ndugu zao wa China katika wakati wote wa shida na raha.
Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping kwa juhudi kubwa alizozichukua yeye na Serikali yake wakiwemo madaktari pamoja na wataalamu wa nchi hiyo katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Katika maelezo hayo, Rais Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo wa China kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa indhari kwa wananchi na kufanya juhudi katika kuhakikisha inajikinga na maambukizo ya virusi vya corona.
Aidha, Rais Dk. Shein aliipongeza taarifa aliyopewa na Balozi huyo ya upatikanaji wa fedha kutoka Benki ya Exim ya China kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wa (Terminal III).
Rais Dk. Shein alisema kuwa ujenzi huo hivi sasa unaendelea na umefikia asilimia 56 baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza ujenzi huo kwa fedha zake za ndani ambapo hadi sasa Serikali imeshamlipa Mkandarasi Kampuni ya BCEG jumla ya Dola za Kimarekani milioni 22 kati ya milioni 58 zilizokubaliwa hapo awali kwa madhumuni ya kumaliza ujenzi huo.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kuwa ujenzi wa mradi huo wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume utakamilika kwa wakati mzuri ambapo utazidi kuimarisha uchumi wa Zanzibar huku akipongeza azma za Serikali ya China ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza mradi huo.