Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na wawekezaji na wamiliki wa makampuni matatu ambayo yameonesha nia ya kuwekeza Zanzibar, yakijumuisha Amazon Real Hubs (usindikaji na usafirishaji wa korosho na bidhaa za matunda), West Avest Company (ufugaji wa kuku na uzalishaji wa mayai), pamoja na Trade Hubs Pharmaceutical (huduma za tiba na utengenezaji wa dawa) kutoka Brazil.
Dkt. Mwinyi amekutana na wawekezaji hao leo tarehe 16 Desemba 2025 Ikulu, Zanzibar, alipokutana nao kwa mazungumzo yaliyojikita katika fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Zanzibar na Brazil.
Ujumbe huo umeongozwa na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Mhe. Gustavo Martins Noguera, akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Dkt. John Stephen Simbachawene. Aidha, mazungumzo hayo yamehudhuriwa na mwenyeji wao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais anayeshughulikia Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Mhe. Hamza Hassan Juma.
