Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amejumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika futari aliyoiandaa kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 05 Machi 2026 katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, na imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa dini pamoja na waumini wa Dini ya Kiislamu, pamoja na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi.

Alhaj Dkt. Mwinyi amewashukuru wananchi wote waliohudhuria katika futari hiyo iliyojumuisha watu wa makundi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu, wajane, mayatima pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwahimiza waumini na viongozi wa Dini ya Kiislamu kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili kudumisha amani iliyopo hapa nchini.

Rais Dkt. Mwinyi amekuwa akiendeleza utaratibu wa kuandaa futari kwa wananchi inayofanyika katika mikoa yote mitano ya Zanzibar wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Mohammed Ali Abdalla, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa mapenzi na upendo wake kwa wananchi anaowaongoza na kumtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake.