RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema miradi ya kimkakati inayoendeshwa Zanzibar inahitaji kuzingatia wakati katika utekelezaji wake ili kuleta tija kwa Taifa.Rais Dk. Mwinyi ameeleza hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na Ujumbe wa watendaji kutoka Kituo cha Nishati cha Oman uliofika kuelezea hatua za miradi wanayoisimamia hapa Zanzibar ukiwemo miradi ya Maji, Nishati na ukarabati wa Mji Mkongwe ambao ni urithi wa dunia.

Rais Dk. Mwinyi ameuhakikishia ujumbe huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itawapa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha miradi hiyo aliyoielezea kuwa na umuhimu mkubwa kwa Uchumi wa Zanzibar, maendeleo na ustawi wa wananchi wake.Dk. Mwinyi ameueleza Ujumbe huo kutosita kuwasilisha Serikalini vikwanzo na changamoto zozote zitakazojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi hiyo ili Serikali ichukue hatua za haraka kukabiliana nazo.

Akitilia mkazo mradi wa maji safi na salama Rais Dk. Mwinyi ameushauri ujumbe huo kuweka mazingatio zaidi kwa kuhakikiksha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa maeneo yote yaliyopitiwa na miradi yao.Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarajika kwake kwa muendelezo na utayari wa utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na kituo cha Nishati cha Oman hapa Zanzibar ambayo inaendelea kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kudumu baina ya Oman na Zanzibar.

Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho, Abdallah Humaid Al Ma’amary alisema, moja ya maboresho ya Mji Mkonge ni kuufanya kuwa mji wa kisasa (Smart City) bila kuharibu uhalisia wa mji huo na kuzingatia vigezo na miongozo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuwa ni urithi wa dunia na kielelezo muhimu cha historia ya Zanzibar. 

Ameeleza kuwa tayari wamekamilisha upembuzi yakinifu kwa miradi wanayotarajia kuitekeleza na kusifu ushirikiano wanaoupata kutoka kwa watendaji wa kuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waliopitiwa na miradi hiyo.