Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekihakikishia Chama cha Mawakili Zanzibar kuwa Serikali inathamini na kuunga mkono kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo ya kuwasaidia wananchi katika masuala ya kisheria. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 09 Aprili 2026, alipokutana na uongozi wa Chama cha Mawakili Zanzibar ulioongozwa na Rais wa chama hicho, Wakili Joseph Shaban Magazi, waliofika Ikulu, Zanzibar.
Hata hivyo, ameshauri uongozi wa chama hicho kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la wanafunzi wa ngazi ya digrii ya sheria wanaoshindwa kuendelea na masomo. Akizungumzia suala la uwekezaji lililowasilishwa na chama hicho kwa kuomba kupatiwa eneo, Rais Dkt. Mwinyi ameitaka taasisi hiyo kulifanyia tathmini ya kina suala hilo na kujipanga vema kabla Serikali haijafanya maamuzi ya kuwapatia eneo la ardhi, ili kuepuka kukaa muda mrefu bila kufanyiwa uwekezaji.
Aidha, amesema kasi ya uwekezaji hapa nchini itakuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na awamu iliyopita, na kwamba Serikali inaangalia upatikanaji wa rasilimali pamoja na mipango bora ya uwekezaji. Rais Dkt. Mwinyi amepongeza uamuzi wa Chama cha Mawakili Afrika Mashariki kufanya mkutano mkuu wa mwaka hapa Zanzibar, na kwamba Serikali, kwa kushirikiana na wadau, itaunga mkono kufanikisha mkutano huo.
Naye Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar, Ndugu Joseph Shaban Magazi, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake na juhudi zake katika kuifungua Zanzibar na kuifanya kuwa kituo bora cha uwekezaji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuikabidhi gari taasisi hiyo, ambayo iliomba katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyopita, kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.
