RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemuapisha Naibu Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) Zanzibar, Kepteni Hussein Mohamed Seif.

Hafla ya uapisho huo ilifanyika ukumbi wa Baraza la Mapinduzi - Ikulu, Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman na Hemedi Suleiman Abdulla.

Kepteni Seif awali alikua Mkuu wa Operesheni na Mipango ya Utendaji KMKM, kabla ya uteuzi wake, Mei 13 mwaka huu.
Amechukua nafasi ya Kepteni Khatib Khamis Mwadini aliekua Naibu wa KMKM awali, ambae kwasasa atapangiwa nafasi nyengine.

Viongozi wengine wa Serikali waliohudhuria hafla hiyo ya uapisho wa Kepteni Hussein ni pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Ahmed Said, Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi (BLM), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ (OR-TMSMIM), Masoud Ali Mohammed, Mkuu wa KMKM, Zanzibar Commodore, Azana Hassan Msingiri na viongozi wengine wa KMKM.