Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar , ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuongeza pensheni kwa wastaafu na kuboresha maisha ya wananachi kwa kuhakikisha hifadhi ya jamii, afya, elimu, makaazi na ajira vinapewa kipaumbele cha juu katika Awamu ijayo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na viongozi wa dini, viongozi wastaafu wa Chama, Serikali na wazee wa Chama Cha Mapinduzi katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Dkt. Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni leo tarehe 14 Septemba 2025.Aidha, Dkt. Mwinyi amesema ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kwa asilimia 7.4 (2020–2025) ni uthibitisho wa uwezo mkubwa wa Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya za kisasa za Mikoa ikiwemo (Mnazi Mmoja, Chake Chake, Mahonda na Mkoa wa Kaskazini), ujenzi wa barabara na bandari za Mangapwani, Mpigaduri, Fumba na Mkoani Pemba.
“Hakutakuwa tena na mwananchi wa Zanzibar atakayelazimika kutibiwa nje ya nchi. Tutaleta huduma bora na za kisasa hapa nyumbani. Vijana watapata ajira kupitia viwanda vipya na bandari zetu zitapunguza gharama za biashara,” – Dkt. Mwinyi.Dkt. Mwinyi amewataka viongozi wa dini na wazee kuendelea kuiombea Zanzibar amani, huku akiwaomba wananchi wote kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuhakikisha maendeleo yanaendelezwa na kasi mpya inaleta mafanikio makubwa zaidi.