RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka waislamu nchini kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu adumishe amani iliopo iliTaifa liweze kupata maendeleo yanayohitajika.

Alhadj Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo katika salamu zake kwa waislamu baada ya kukamili sha Ibada ya Sala ya Ijumaa, iliofanyika Masjid Munnawar uliopo Polisi Chumbuni , Wilaya ya Magahribi ‘A’ Unguja.

Amesema ili Taifa liweze kupata maendeleo yanayohitajika, waislamu wana wajibu wa kumuomba Mwenyezi Mungu , alijaalie kila heri na kudumisha amani iliopo.

Aidha, amewataka waislamu kuiombea dua nchi pamoja na Viongozi wake ili waweze kufanikisha dhamira ya kuliletea Taifa maendeleo.

Alhadj Dk. Mwinyi amekubali ombi la waumini wa mskiti huo la kusaidia upatikanaji wa Mazulia mapya kwa ajili ya kuswalia.

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, aliwasisitiza waislamu kuzingatia sifa na taratibu za kisheria katika kuchinja wanyama kuelekea Idd el Adh-ha kwa kuwa jambo hilo ni la Ibada.

Aliwataka waislamu kuepuka kuchinja wanyama wenye ila au wenye athari na akatumia fursa hiyo kuelezea umuhimu wa kuchinja wanyama wenye sifa (vigezo) na afya njema.

“ Kuchinja ni wajibu wa kila muislamu mwenye uwezo, hii ni amri ya Mwenyezi Mungu”, alisema.

Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Simai Juma Ali aliwaeleza waislamu Ubora wa siku kumi (10) za mwezi wa Mfunguo tatu pamoja na fadhila zake na kuwataka kuongeza juhudi kumcha Mwenyezi Mungu, kwa kuzidisha ibada ya Sala za Sunna, kusoma sana Qoraan, pamoja na kuwaombea dua wazazi, viongozi na Taifa kwa ujumla.

Sheikh Khalid alitumia fursa hiyo kuwakumnbusha waislamu wajibu walionao katika kuchinja kwa mujibu wa muongozo wa Dini ya Kiislamu.

Aidha, akasisitiza haja ya waislamu kushiriki Ibada ya sala ya Idd el Hajj kwa mujibu wa utaratibu.

Wakati huo huo, Alhad Dk.Mwinyi alifika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja kuwajuulia hali wagonjwa waliolazwa Hospitalini hapo, ikiwa ni utamaduni wake aliojiwekea.

Miongoni mwa wagonjwa hao ni pamoja na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto Nassor Ahmeid Mazrui pamoja na wagonjwa wengine wanaosumbuliwa na maradhi mbali mbali,.