RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,  amesisitiza kwamba uwamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa mradi wa ujenzi wa hospitali mpya ya Binguni uko pale pale na unatarajiwa kuanza hivi karibuni.Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Afya wakati ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2019/2020, na Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021.Dk. Shein alisema kuwa utekelezwaji wa mradi huo utafanywa kwa kutumia fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba hivi karibuni ujenzi utaanza ambapo Wizara ya Fedha na Mipango itatoa fedha kwa ajili ya kaunza ujenzi huo ambao utakuwa wa aina yake.Alisema kuwa Hospitali hiyo ya kisasa itakayokuwa na majengo kumi na moja, ni mwelekeo wa Serikali katika ujenzi wa hospitali mpya ya kufundishia huko Binguni, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Aliongeza kuwa Serikali imeshaamua kutekeleza ujenzi huo kwani mradi huo umo katila Ilani ya Chama Cha Mapainduzi (CCM), Sera na Mipango na kwamba yeye kwa upande wake ameshaamua kujengwa huku akisisitiza haja ya kuzidisha mashirikiano ili ujenzi huo uwe wa mafanikio.Aliipongeza Wizara hiyo ya Afya kwa uwasilishaji wa Mpango kazi huo sambamba na utekelezaji wake na kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo kwa kufanya kazi zao vyema katika kuwahudumia wananchi.

Rais Dk. Shein alielezea dhamira yake ya kuendelea kutoa ushirikiano na Wizara hiyo ya Afya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiamini kwamba hilo ni jukumu lake kwani kwa Zaidi ya miaka 52 ya maisha yake amekuwa akifanya kazi Serikalini akiwatumikia wananchi.Alisema kuwa viongozi wa Wizara ya Afya wanaopenda kufanya kazi na wamekuwa na mashirikiano makubwa huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Wizara hiyo pamoja na viongozi wengine kwa kutoyumba katika kipindi cha maradhi ya Corona.

Rais Dk. Shein alisema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona hapa nchini yametokana na kujiamini, kutoogopa na kuondoa hofu sambamba na kuwa wamoja.Aidha, alisisitiza kuwa wafanyakazi wa sekta ya afya wana kazi kubwa ya kutoa huduma kwa wananchi na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kwamba huduma za afya kwa Zanzibar kuwa bure.Aliwataka wafanyakazi wa Wizara ya Afya kuendelea kuyasimamia maamuzi ya Serikali kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaendelea kutolewa bure na kusisitiza kuwa hakuna haja ya wananchi kuambiwa vyenginevyo wanapotaka huduma za afya.

Kadhalika, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kufanya tafiti ili kuimarisha sekta hiyo, kwani alisema suala la utafiti ni uwamuzi wa dunia nzima ambao umekuwa ukisaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo.Akizungumzia vikao vya kutathmini utekelezaji wa mpango kazi ambavyo vimekuwa vikifanyika katika kipindi chote cha uongozi wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema kuwa vikao hivyo (bango kitita) ambavyo ni vya mwisho katika muda wa uongozi wake, vimemsaidia kwa kiasi kikubwa kufuatilia utekelezaji wa mipango ya Serikali katika Wizara zake.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uwasilishwaji Mpango Kazi huo iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa viongozi kuhakikisha wafanyakazi wao wanafanya kazi ipasavyo katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu mnamo mwezi wa Oktoba mwaka huu.Mapema Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed aliyaelezea miongoni mwa mafanikio yaliopatikana katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi ambapo jumla ya wafanyakazi wapya 771 wa kada mbali mbali wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wa maabara wameajiriwa na wafanyakazi 164 wamepelekwa masomoni ndani na nje ya nchi wakiwemo madaktari bingwa 31.

Aliongeza kuwa mafanikio mengine ni kukamilika kwa muundo wa utumishi wa kada za afya, kukamilika kwa jengo la huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Kivunge, kuendelea kuimarisha kwa upatikanaji wa dawa muhimu katika hospitali na vituo vya afya zikiwemo za saratani na za kusafisha figo.Mafanikio mengine ni kukamilika kwa Bohari Kuu ya dawa Pemba, upatikanaji wa mashime ya “PCR” ya kupimia magonjwa mbali mbali ikiwemo Corona, kuanzishwa kwa kliniki maalum ya huduma za wagonjwa waliopandikizwa figo katika hospitali ya MnaziMmoja ambapo jumla ya wagonjwa sita wanaendelea na huduma hizo.

Pia, ni kukamilika kwa jengo la macho katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Ununuzi wa CT Scan mpya yenye uwezo mkubwa wa uchunguzi wa maradhi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, ufungwaji wa tanuri jipya la kuchomea taka pamoja na upatikanaji wa vifaa muhimu vya huduma za mifupa ikiwemo kitanda maalum cha upasuaji wa mifupa na X-ray inayotumika wakati wa upasuaji.

Nao viongozi wa Wizara hiyo walimpongeza Rais Dk. Shein kwa maelekezo yake anayoyatoa kwao hatua ambayo imewarahisishia kutenda kazi zao kwa ufanisi mkubwa na kupelekea sekta ya afya kupata mafanikio makubwa sana hapa nchini.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati alitoa pongezi kwa uongozi na wafanyakazi wake wote kwa kufanikisha vyema kazi za Wizara hiyo ikiwemo uwasalishaji wa utekelezaji wa Mpango Kazi huo.Rais Dk. Shein alisema kuwa vikao hivyo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kwani watendaji wameweza kujipima wenyewe na kusisitiza haja ya kuviendeleza hasa katika ngazi za Wizara huku akieleza matumaini yake kwa Wizara hiyo.

Nae Naibu Waziri wa Wizara hiyo Juma Makungu Juma alieleza kuwa Wizara inaendeleza juhudi na Mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kuwa wananchi kwa ujumla wao wanapata huduma bora za maji, nishati iliyo salama na endelevu, makaazi bora na matumizi mazuri ya ardhi yenye kuzingatia mahitaji ya sasa na baadae.

Rais Dk. Shein pia, katika vikao vyake vya leo alikutana na uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda chini ya Waziri wake Balozi Amina Salum Ali ambapo Waziri huyo alieleza kuwa Wizara katika mwaka 2020/2021 inatarajia kuandaa Mpango wa matumizi na upembuzi yakinifu kwa eneo la Dunga.Aidha, alisema kuwa Wizara inakusudia kuliandaa kwa ajili ya ubia eneo la Nyamanzi wka hatua za awali kufanya tathmini ya kimazingira na kijamii (ESIA) pamoja na kulisafisha.

Kwa upande wa Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC), Shirika hilo limefanikiwa kuzindua mtambo mpya wa uzalishaji wa mafuta ya Mikaratusi katika kiwanda cha mafuta ya Makonyo na Arki za mimea huko Wawi Pemba.Alisema kuwa Wizara kupitia Shirima hilo la (ZSTC) inatarajia kuanzisha kiwanda cha kusarifu mwani katika eneo la Chamanangwe Pemba kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Indonesia.