Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema fedha zilizopo katika Akaunti Maalum ya Kulipia Madeni zimefikia Dola za Kimarekani Milioni 350. Dkt. Mwinyi amesema hatua hiyo imeiwezesha Zanzibar kukopesheka kwa kuweza kulipa madeni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 27 Oktoba 2025, baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi mikubwa mitatu ya kimkakati katika hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar.

Mikataba hiyo inahusisha ujenzi wa miradi mitatu mikubwa ya kimkakati ambayo ni Ujenzi wa Taasisi ya Saratani Binguni, Mradi wa Usambazaji Maji Mkoa wa Kusini Unguja, na Mradi wa Mfumo Jumuishi wa Usimamizi na Usajili wa Huduma za Ardhi Zanzibar (LARIS). Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafarijika kuona mpango mzuri wa kupata fedha za kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani.

Amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa Zanzibar kwa kuwa imeweza kutekeleza miradi mikubwa mitatu kwa pamoja yenye jumla ya gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 150 kupitia taasisi za fedha za ndani. Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa Zanzibar inakopesheka kwa sababu ina utaratibu maalum wa kujiwekea akiba katika Akaunti Maalum ya Kulipia Madeni, ambapo kila mwezi huweka akiba ya Dola za Kimarekani Milioni 15, sawa na Dola Milioni 180 kwa mwaka. Amesema utaratibu huo unaiongezea Serikali uwezo wa kulipa madeni na kuaminika zaidi na taasisi za kifedha.

Akizungumzia miradi mitatu iliyotiwa saini, Dkt. Mwinyi amesema miradi hiyo itamaliza changamoto tatu kubwa zilizodumu kwa muda mrefu: ukosefu wa maji katika Mkoa wa Kusini Unguja, migogoro katika sekta ya ardhi kupitia mradi wa LARIS, na gharama kubwa za matibabu ya saratani ambapo sasa wagonjwa watapata huduma ndani ya nchi. Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuwa na hospitali zinazotoa huduma za afya kwa ushindani, ili kila mwananchi aweze kupata matibabu bora kwa wakati.

Aidha, amefahamisha kuwa Serikali inalenga kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na Bima ya Afya, hatua itakayowezesha kufikiwa kwa sera ya Afya kwa Wote. Rais Dkt. Mwinyi pia ametoa rai kwa watendaji wa Serikali na wadau wa maendeleo kuondoa urasimu katika majadiliano ya miradi kabla ya utekelezaji wake, akisema ucheleweshaji huo unadhoofisha kasi ya maendeleo. Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru washirika wa maendeleo, hususan taasisi za fedha za ndani, kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa mitatu.

Mkataba wa Mradi wa Mfumo Jumuishi wa Usimamizi na Usajili wa Huduma za Ardhi Zanzibar (LARIS) ulitiwa saini kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Ndg. Abdulmajid Mussa Nsekela, na Makamu wa Rais wa Kitengo cha Ufadhili wa Biashara wa BPI France, Bi. Alienor Daugreilh. Kwa upande wa Mradi wa Usambazaji Maji Mkoa wa Kusini Unguja, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Ndg. Joseph John Kilangi, na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Next Health Digital Solution BV kutoka Uholanzi.

Aidha, Mkataba wa Ujenzi wa Kituo cha Huduma za Saratani Binguni ulitiwa saini kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, na Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi wa Kituo cha Aegle Onco Care Center Limited, Dkt. Diara Pankaj Wadhwa. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya Salum, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa maono yake yaliyoiwezesha Zanzibar kupiga hatua kubwa za kiuchumi, na kufanikisha utekelezaji wa miradi mingi mikubwa ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani.

Mkataba wa Mradi wa Mfumo Jumuishi wa Usimamizi na Usajili wa Huduma za Ardhi Zanzibar (LARIS) ulitiwa saini kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Ndg. Abdulmajid Mussa Nsekela, na Makamu wa Rais wa Kitengo cha Ufadhili wa Biashara wa BPI France, Bi. Alienor Daugreilh. Kwa upande wa Mradi wa Usambazaji Maji Mkoa wa Kusini Unguja, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Ndg. Joseph John Kilangi, na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Next Health Digital Solution BV kutoka Uholanzi.