Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amejumuika na waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba katika futari ya pamoja aliyowaandalia. Hafla hiyo imefanyika leo, tarehe 12 Machi 2026, katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, na imehudhuriwa pia na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi.

Rais Dkt. Mwinyi amewaomba kuendelea wananchi hao kuwaombea dua viongozi wakuu wa nchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kukabiliana na changamoto zinazoibuka, hasa katika ulimwengu wa sasa uliojaa majanga mbalimbali yanayotishia amani ya dunia, pamoja na kuiombea nchi amani.

Futari hiyo imewajumuisha watu wa makundi mbalimbali, wakiwemo mayatima, wajane, watu wenye ulemavu, walimu wa madrasa, masheikh na maimamu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa dini ya Kiislamu, Sheikh Maalim Mkashari amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa wema anaowafanyia wananchi wake, na kumuelezea kuwa ni kiongozi mwema anayetenda mema kwa anaowaongoza. Aidha, ameeleza kuwa kufutarisha ni kitendo adhimu chenye baraka na thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.