Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amempongeza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ndg. Abdi Mahmoud Abdi, kwa uteuzi wake na kumtaka kutekeleza majukumu yake kwa bidii, huku akiahidi kumpatia ushirikiano zaidi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 19 Agosti 2026, alipokutana na Ndg. Abdi Mahmoud Abdi, aliyefika Ikulu Zanzibar kujitambulisha rasmi kufuatia uteuzi wake kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, pamoja na kupokea maelekezo kuhusu utekelezaji wa majukumu yake mapya.
Amesema ana imani na uwezo wake kutokana na uzoefu na utendaji aliouonesha alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na viongozi na watendaji wa Chama katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Ndg. Abdi Mahmoud Abdi amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa ushauri na maelekezo aliyompatia, na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na viongozi na watendaji wenzake katika kutekeleza majukumu ya Chama.
