Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ushirikiano wa kimahakama wa kikanda ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki, kubadilishana uzoefu na kuhakikisha Mahakama zinaendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 05 Oktoba 2026, wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), uliofanyika Verde Hotel, Zanzibar.
Amesema Mahakama zinapaswa kukumbatia ubunifu na teknolojia katika kuboresha huduma za haki, huku zikilinda misingi ya haki, usawa na taratibu stahiki za kisheria.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa uhuru wa kifedha wa Mahakama, akieleza kuwa upatikanaji wa rasilimali za kutosha na zinazotabirika ni msingi wa Mahakama kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya kikatiba.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amezindua nyaraka tatu muhimu za Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF).
Mkutano huo umewakutanisha Majaji Wakuu na viongozi wa Mahakama kutoka nchi 15 za Afrika kwa ajili ya kujadili ubunifu, ufanisi na mageuzi katika usimamizi wa Mahakama na utoaji wa haki.
.jpeg)