Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo, tarehe 18 Julai 2026, ameendelea na ziara yake ya kikazi nchini India kwa kutembelea Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), jijini Chennai.Kituo hicho kinawaunganisha wanataaluma, watafiti, wanafunzi, mampuni na ujasiriamali katika kubuni na kuendeleza teknolojia zinazolenga kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Akiwa katika kituo hicho, Rais Dkt. Mwinyi ameongozwa na Mkuu wa IIT Madras, Prof. V. Kamakoti, pamoja na viongozi na wataalamu wa taasisi hiyo, ambao wamemweleza kuhusu tafiti, shughuli na programu mbalimbali za ubunifu zinazoendeshwa katika kituo hicho.Rais Dkt. Mwinyi pia ametembelea IITM Pravartak Technologies Foundation, kitovu cha uvumbuzi wa teknolojia kinachohusishwa na IIT Madras, ambacho kinaendeleza tafiti, ujuzi na suluhisho za kiteknolojia katika maeneo ya akili mnemba, mifumo ya mawasiliano, usalama wa kimtandao na mifumo ya udhibiti.

Baada ya kupokea maelezo kuhusu shughuli hizo, Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru IIT Madras kwa fursa zinazotolewa kwa Zanzibar, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuwawezesha vijana, kukuza vipaji na ubunifu, pamoja na kuwajengea uwezo wa kutumia maarifa na teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.

Aidha, Taasisi ya Teknolojia ya India Madras inatarajiwa kuzindua rasmi tarehe 10 Agosti 2026 programu ya kimataifa ya mafunzo ya wiki sita yatakayofanyika Zanzibar. Programu hiyo itawahusisha washiriki kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo Wazanzibari, na inalenga kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa katika ukaguzi, udhibiti na usimamizi wa fedha, hususan katika maeneo ya mifumo ya kidijitali, sayansi ya data, akili mnemba na usalama wa kimtandao.

Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameambatana na Mkewe, Mhe. Mama Mariam Mwinyi; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe; Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Kapufi Mbega; pamoja na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kuondoka jijini Chennai leo kuelekea New Delhi, baada ya kukamilisha shughuli zake katika Taasisi ya Teknolojia ya India Madras