Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewatembelea wagonjwa kutoka Zanzibar wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya MIOT International, jijini Chennai, nchini India, kupitia udhamini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amefanya ziara hiyo leo, tarehe 18 Julai 2026, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi nchini India, kwa lengo la kuwajulia hali wagonjwa hao na kufahamu maendeleo ya matibabu wanayoendelea kupatiwa.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Dkt. Mwinyi amezungumza na wagonjwa pamoja na familia zao na kupokea maelezo kutoka kwa madaktari kuhusu hali zao za afya, hatua zilizofikiwa katika matibabu na huduma za kibingwa wanazopatiwa.

Miongoni mwa wagonjwa waliotembelewa na Rais Dkt. Mwinyi ni Abdallah Bakari Abdallah (18), kijana kutoka Makachu anayepatiwa matibabu katika Kitengo cha Tiba ya Viungo katika hospitali hiyo, ambaye hali yake inaendelea kuimarika.

Abdallah ameeleza kufurahishwa na kutimia kwa ndoto yake ya kukutana na Rais Dkt. Mwinyi na kumshukuru kwa kumtembelea, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kumpatia fursa ya kupokea matibabu nchini India.

Ziara hiyo pia imeonesha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za afya nchini India, ili kupanua fursa za upatikanaji wa huduma za kibingwa na bobezi kwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amepata fursa ya kukutana na madaktari bingwa wanaoendelea na programu ya SET kupitia Mpango wa Mama Samia Scholarship.

Rais Dkt. Mwinyi amepokea maelezo kuhusu mafunzo yao, maeneo ya utaalamu wanayosomea na namna maarifa na ujuzi watakaoupata utakavyosaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.

Programu hiyo inalenga kuongeza idadi ya wataalamu wa afya wenye utaalamu wa juu, kuimarisha uwezo wa hospitali nchini kutoa huduma za kibingwa na bobezi, pamoja na kupunguza ulazima wa kupeleka wagonjwa wengi nje ya nchi kwa matibabu.