Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na mfumo madhubuti wa matumizi na usimamizi bora wa ardhi, ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali hiyo na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 28 Juni 2026, katika kilele cha Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Ardhi na Makaazi, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Serikali imeamua kuanzisha Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi na Makaazi kutokana na umuhimu mkubwa wa sekta hizo katika maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi, hususan kwa Zanzibar ambayo ni nchi ya visiwa inayokabiliwa na changamoto ya ufinyu wa ardhi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii katika mataifa yote duniani. Kutokana na umuhimu wake, ardhi ni suala mtambuka linalogusa sekta zote, hivyo ni lazima itumiwe na kusimamiwa kwa uangalifu ili kuleta maendeleo endelevu.
Aidha, amesema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi ina jukumu kubwa la kuisimamia sekta hiyo kwa kuhakikisha ardhi yote inatambuliwa, inapimwa, inapangiwa matumizi, inasajiliwa na kutolewa hati za matumizi ya ardhi kwa wanaostahiki.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali tayari inatekeleza mradi mkubwa wa usimamizi na usajili wa ardhi nchini, ambao umeanza vizuri kwa kujenga vituo vitano vya taarifa za ardhi katika kila mkoa.
Amesema mradi huo pia unahusisha uandaaji wa rejea sahihi za vipimo vya upimaji, ukusanyaji wa taarifa za msingi za ardhi na ubadilishaji wa taarifa pamoja na nyaraka za ardhi kutoka katika mfumo wa kawaida kwenda katika mfumo wa kidijitali.
Vipengele vingine vya mradi huo ni kuanzishwa kwa Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Ardhi, usimamizi wa mabadiliko, kuwajengea uwezo watendaji, utambuzi na usajili wa ardhi pamoja na matengenezo na uendeshaji wa mifumo hiyo.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatarajia kuwa mradi huo utakapokamilika, utasaidia kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mipango thabiti ya matumizi ya ardhi na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Amesema mradi huo pia utaiwezesha Zanzibar kuwa na rasilimali ya ardhi inayotambuliwa, iliyopimwa, iliyopangiwa matumizi na kusajiliwa rasmi. Hatua hiyo italeta mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi na kuimarisha usimamizi pamoja na matumizi bora ya rasilimali hiyo.
Akizungumzia Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi na Makaazi, Rais Dkt. Mwinyi amesema maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo, kutoa elimu kwa wananchi, kujadili mafanikio na changamoto zilizopo pamoja na kutafuta ufumbuzi wake.
Ameipongeza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kwa kuendelea kuyaratibu maadhimisho hayo kwa mafanikio kwa mwaka wa pili mfululizo.
Rais Dkt. Mwinyi amesema ni lazima Serikali ipange kwa umakini ardhi iliyopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo kilimo, viwanda, masoko, uwekezaji, huduma za jamii, viwanja vya michezo, miundombinu ya maji na umeme, huduma za mawasiliano, makaazi na biashara.
Amesema wananchi wengi, hususan vijana, wanahitaji maeneo ya kujenga nyumba za kuishi, wakati ardhi iliyopo ni ndogo, haiongezeki na inaendelea kupungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Wakati huo huo, idadi ya watu inaendelea kuongezeka na inakadiriwa kufikia takribani watu milioni 3.6 Zanzibar ifikapo mwaka 2050.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba bora na salama za makaazi zitakazowezesha idadi kubwa ya watu kuishi katika eneo dogo la ardhi.
Ameeleza kuwa nyumba 548 zinajengwa katika eneo la Kisakasaka B, nyumba 1,095 Kikwajuni, nyumba 1,095 Chumbuni na nyumba 22 katika eneo la Mombasa kwa Awamu ya Pili. Miradi mingine ni pamoja na Jengo la Biashara la Maisara na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mengine ya Unguja na Pemba
.jpeg)