Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa atahakikisha sekta ya michezo inaimarika zaidi katika kila nyanja ili Zanzibar irudi katika asili yake ambapo Zanzibar ilitambulikana ndani na nje ya bara la Afrika katika sekta hiyo.Dk. Shein alisema kuwa tayari kwa upande wa Serikali Idara maalum imeshaundwa kwa ajili ya kushughulikia michezo ikiwa na lengo la kuiimarisha sekta hiyo hapa nchini.Aidha, Dk. Shein alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha vuguvugu la michezo linaimarika sambamba na kuwapa kipaumbele wanafunzi ili nao wawe na muda wa kushiriki michezo.

Dk. Shein alisisitiza kuwa michezo kwa vijana na watoto wa skuli ina umuhimu mkubwa katika kuwajenga kiafya, kiakili pamoja na kuwajenga watoto na vijana kujenga ushirikiano, upendo na umoja miongoni mwao.
Kutokana na umuhimu huo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kuwataka wazee kutowazuia watoto wao kushiriki michezo kutokana na umuhimu wake mkubwa katika maisha ya mwanaadamu.Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa sekta ya michezo katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaimarishwa kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka (2015-2020) ambapo Serikali itatekeleza mambo kadhaa kwa lengo la kuiimarisha sekta hiyo.

Katika uongozi wa Dk. Shein Serikali imetekeleza mambo mbali mbali katika kuimarisha sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Sera mpya ya michezo ya Zanzibar itakayoimarisha na kuiendeleza michezo yote.Aidha, Serikali imeanzisha mashindano ya riadha ya Wilaya, kwa Wilaya zote kumi za Zanzibar pamoja na kutoa vifaa mbali mbali vya michezo kwa wanariadha wa Zanzibar ili kurejesha vuguvugu la michezo ya riadha ambapo bado utaratibu wa kutoa vifaa hivyo unaendelea.

Pamoja na hayo, Serikali imewahamasisha wananchi waendeleze michezo ili wajenge afya zao kwa kufanya mazoezi ya viungo kila siku sambamba na kushiriki kwenye tamasha la mazoezi ya viungo linalofanyika tarehe 1 Januari ya kila mwaka.