RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi aliwataka waumini wa dini ya kiislam kuitumia misikiti kuwa jukwaa la kuchota elimu zenye manufaa kwa jamii pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa msikiti wa masjid Salim, Sogea mjini Unguja, alipojumuika na waumini wa Kiisaam kwenye sala ya Ijumaa.
Alisema misikiti haipo kwa lengo la kutekelezwa ibada ya sala pekee, bali ikiitumiwa vizuri ni sehemu bora ya kutafuta ufumbuzi wa chamgamoto zinazoikabili jamiii.Alisema bado jamii haioni umuhimu wa kuitumia misikiti kama sehemu ya kukutana na kuelezana matatizo yao ambayo ni mengi na yanahitaji ufumbuzi wa haraka, hivyo aliwaasa kuitumia kwa kujua yanayoendelea kwenye jamii zao ili kutafuta namna ya kuwasaidia.
“Katika kutumia misikiti yetu si kusali tuu, bali kuzungumza masuala ya kijamii, kutafuta utatuzi wa changamoto katika jamii zetu, tumeambiwa hapa kuna wajane wengi, kuna watoto yatima, matatizo ya maji, kuna misikiti kwa kuweka shura wametatua changamoto nyingi ikiwemo kuchimba visima vya maji” alifahamisha Rais Mwinyi.
Aidha, aliwahimiza waumini hao kujitokeza kwa wingi misikiti kwa sala na siku zote sio kwa Ijumaa pekee.“Hata hili la kusali bado ni changamoto utakuta Ijumaa watu hujaa tele misikitini lakini siku za kawaida safu moja wakati mwengine hata safu haitimii, tuhimizane watu tusali, hii misikiti inajengwa watu wasali” alihimiza.Sambamba na hilo Al hajj Mwinyi aliwasihi waumini hao kuitumia vyema misikiti kwa kuitunza na kuwa tayari kurekebisha itakapoharibika ama kuhitajika marekebisho.
Alisema misikiti itahitaji kuhudumiwa kwa umeme, ukarabati kwa sehemu zitakazochakaa ama kuharibika ikiwemo kupakwa rangi na vifaa vyengine muhimu endaapo vitaharibika.“Msikiti huu utahitaji kutunzwa, utahitaji maji, umeme, kunahitaji kurekebishwa mifereji itakayoharibika, msikiti unahitaji usafi, utahitaji kukarabatiwa, rangi ikichakaa itahitaji iwekwe nyengine na hapa ndipo penye matunzo yenyewe ili kuifanya misikiti yetu idumu, wito wangu kwa waumini wenzangu kwa kila mwenye uwezo ajitolee kuchangia kwa kadri ya hali itakavyoruhusu” Alinasihi Al hajj Mwinyi
Aidha, aliwahimiza waumini hao kujitolea kwa kila mwenye uwezo kadri ya hali itakavyowaruhusu ili misikiti iendelee kudumu.Alisema misikiti mizuri haitobakia na uzuri wake isipotunzwa, hivyo aliwanasihi waumini kuendelea kuitunza kwa kuihudumia kadri itakavyohitaji.Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwakilishi jimbo la Magomeni Jamaal Kassim Ali ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, alieleza kukamilika kwa ujenzi wa msikiti huo kulisaidiwa sana na ushirikiano mzuri walioupata kutoka ofisi ya Mufti pamoja na juhudi za wananchi wa jimbo lake, mbali na nguvu kutoka kwa mfadhili.
Naye, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume wakati akihutubu kwenye sala ya Ijumaa aliwanasihi waumini wa msikiti huo kutoshindana na nafsi zao kwenye masuala ya jamii badala yake aliwataka kurejea kwenye mafundisho ya Mtume (SAW) kwa kutatua matatizo yao kwa njia za shura misikitini.
Mapema akizungumza kwenye rislala ya waumini wa msikiti huo, Mudathir Abdalla alisema Masjid Salim ulijingwa tokea mwaka 1998 na mwaka mmoja baadae uliboreshwa kwa kuanza kusaliwa sala ya Ijumaa hadi mwaka 2021 ulipata mfadhili kupitia Mwakilishi wa jimbo lao (Magomeni) Jamaal Kassim Ali na kujengwa upya ambapo kwasasa ni msikiti mkubwa na wenye hadhi ya hali ya juu.