Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametunuku Nishani ya Mapinduzi na Nishani ya Utumishi Uliotukuka kwa Viongozi na Wananchi mbalimbali wenye sifa maalum waliotoa mchango mkubwa katika historia, maendeleo na ustawi wa Zanzibar.
Akisoma Tamko la Kwanza la Kutunuku Nishani hizo, Katibu Mkuu wa Afisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Ndg. Saleh Juma Mussa, amesema jumla ya watu 18 wametunukiwa Nishani hizo, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao wa kipekee kwa Taifa.
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 11 Januari 2026 katika Viwanja vya Ikulu, Mjini Zanzibar, na kuhudhuriwa na Viongozi wa Kitaifa, Viongozi wa vyama vya siasa, Watendaji Wakuu wa Taasisi za umma, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi mbalimbali.
Tukio hilo ni miongoni mwa shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Waliotunukiwa Nishani ya Mapinduzi ni pamoja na:
1.Mama Fatuma Karume – Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
2.Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Bin Omar Bin Kaab Bin Ahmed Baalawiy.
3.Marehemu Sheikh Hassan Bin Ameir Al-Shirazy.
4.Marehemu Sheikh Mussa Makungu Ali.
5.Marehemu Askofu John Ackland Ramadhani.
6.Profesa Jose Piquer.
7.Ndugu Gulam Abdalla Rashid.
8.Marehemu Bimvita Mussa Kibendera.
Waliotunukiwa Nishani ya Utumishi Uliotukuka ni pamoja na:
9.Brigedia Jenerali Said Hamis Said.
10.Kamishna wa Polisi (CP) Kombo Khamis Kombo.
11.Kamishna wa Uhamiaji (CI) Hassan Ali Hassan.
12.Commodore Azana Hassan Msingiri.
13.Kanali Makame Abdallah Daima.
14.Kamishna Rashid Mzee Abdallah.
15.Kamishna Khamis Bakari Khamis.
16.Kanali Burhani Mzee Nassor.
17.Luteni Kanali Said Ali Shamhuna.
18.Ndugu Ali Abdalla Ali.
Nishani ya Mapinduzi hutolewa kwa mtu aliyeasisi, kushiriki au kuyatukuza Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, au kwa kiongozi au mtu mwingine (aliye hai au aliyefariki) aliyeiletea Zanzibar heshima na sifa katika fani mbalimbali, pamoja na kuonesha maadili mema yanayostahili kuigwa.
Kwa sasa, Wazanzibari wanaendelea kuadhimisha Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa shamrashamra na matukio mbalimbali ikiwemo ufunguzi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, kuelekea kilele cha Siku ya Mapinduzi tarehe 12 Januari 2026.