Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ndoto ya Zanzibar ya kujitosheleza katika uzalishaji wa kuku hapa nchini imetimia, hatua ambayo itaipunguzia nchi utegemezi wa kuagiza kuku kutoka nje. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 8 Disemba 2026, alipoufungua rasmi Mradi wa Shamba la Ufugaji wa Kuku wa Zan Breed Limited, uliopo Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesisitiza kuwa uzalishaji huo ni lazima uwalenge na uwasaidie wafugaji wadogowadogo, kwa kuwajengea uwezo ili nao wanufaike moja kwa moja na fursa zinazotokana na uwekezaji huo mkubwa. Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Mradi wa Zan Breed ni muhimu katika kuwawezesha wafugaji wadogowadogo kwa kutoa elimu ya ufugaji, kuchangia upatikanaji wa vifaranga bora na chakula cha kuku kwa bei nafuu, pamoja na huduma za chanjo na masoko ya uhakika kwa wafugaji wa ndani.

Akizungumzia mradi huo, Rais Dkt. Mwinyi ameuelezea kuwa ni mradi mkubwa wa kimkakati, unaoonesha kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kwa kuanza kuwa na miradi mikubwa ya kimataifa ya aina hiyo. Amesema hali hiyo inaonesha wazi kuwa nchi haina sababu ya kuendelea kuagiza kila bidhaa kutoka nje. Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuwalinda wawekezaji wa ndani kwa kuweka sera za kifedha na kodi zitakazowapa unafuu, tofauti na zile za wawekezaji kutoka nje, ili kuwajengea uwezo wa kuhimili ushindani.

Ameongeza kuwa ni lazima kuwepo sera mahsusi za kifedha kwa ajili ya kulinda viwanda vya ndani na bidhaa zinazozalishwa nchini, kwa lengo la kuinua mitaji ya wawekezaji wa ndani na kukuza uchumi wa taifa.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi ameiagiza Wizara ya Uwezeshaji kuhakikisha wafugaji wadogowadogo wanawezeshwa kupitia mikopo isiyo na riba, mafunzo ya ufugaji, upatikanaji wa chakula cha kuku, vifaranga bora pamoja na masoko ili kuhakikisha wanapata faida stahiki. Amesema Serikali itaendelea kutoa mikopo nafuu kwa wafugaji ili kuinua mitaji yao, na kuiagiza Wizara ya Kilimo kuutumia Mradi wa Zan Breed kama mwanzo wa kuwawezesha wafugaji wadogowadogo kote Zanzibar.

Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Ndugu Saleh Saad, amesema mradi huo una mtaji wa Dola za Marekani Milioni 105, na unatarajiwa kutoa fursa za ajira zaidi ya 1,000. Ameongeza kuwa mradi huo una uwezo wa kuzalisha kuku 800,000 kwa mwezi, sambamba na kutoa huduma za kliniki ya kuku, kiwanda cha nafaka, maabara ya kuku pamoja na mfumo wa kuchakata maji, hatua itakayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya mifugo na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.