RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ataendeleza utamaduni wa muda mrefu wa kuwafutarisha wananchi katika Mikoa yote ya Zanzibar kila mwaka, kwani hilo ni jambo jema na lenye manufaa.Alhaj Mwinyi amesema hayo katika hafla ya futari aliyoiandaa kwa wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, iliofanyika katika Ukumbi wa Michenzani Mall, jijini Zanzibar.
Akitoa shukrani kwa wananchi hao, alisema amefurahishwa na hatua yao ya kuitikia wito wake na kujumuika pamoja katika futari hiyo.Aliwatakia kheri na malipo mema kwa Mwenyezi Mungu wananchi hao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharini, Idrissa Kitwana Mustafa, alimshukuru na kumtakia kheri Alhaj Dk. Mwinyi kwa hatua yake ya kuwaunganisha wananchi.
Aidha, aliwashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kuitikia wito wa Rais wa Zanziar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Mwinyi na kuwataka kuendelea kumuombea dua na kheri kwa Mwenyezi Mungu ili amfanyie wepesi katika kazi zake.
Mapema, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume alisema utaratibu unaoendelea kufanyika wa kuwafutarisha wa mikoa mbali mbali hapa nchini una lengo la kuwaweka pamoja wananchi.
Hafla hiyo ya futari imewajumuisha wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi kutoka makundi mbali mbali, ikiwemo Masheikh, wanazuoni, wawakilishi wa vyama vya siasa, mayatima, watu wenye ulemavu na wengineo