RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema madhumuni ya Binaadamu kuletwa Ulimwenguni ni kumuabudu Mwenyezi Mungu, hivyo amesisistiza wajibu wa waislamu kujifunza Dini yao pamoja na kuwafunza watoto wao.Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo katika Ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa ‘Masjid Hussein’ ulioko Ghana Kichakani, Wilaya Kati Unguja, hafla iliokwenda sambamba na Ibada ya sala ya Ijumaa.
Amesema dhamira ya Binadamu kuletwa Ulimwenguni, ni kumcha Mola wake pamoja na kuwafunza watoto elimu ya Dini ili waweze kutekeleza Dini yao kwa usahihi kama ilivyoamrishwa.Alieleza kuwa suala la kutafuta elimu ni muhimu na lenye manufaa makubwa Duniani na akhera, hivyo akaunga mkono azma ya waumini wa msikiti huo ya kuendeleza elimu ya dini na kusema ni jambo jema.
Alhaj Mwinyi aliahidi kuchangia ujenzi wa Madrsa katika eneo la pembezoni mwa msikiti huo pamoja na kufanikisha ujenzi wa uzio kuzunguka msikiti huo.Aliwashukuru waumini na Viongozi wao kwa hatua yao ya kuiita msikiti huo jina lenye mnasaba na jina lake la ‘Hussein Aidha aliwataka waumini kuendeleea kuutunza na kuufanyia matengenezo ya mara kwa mara msikiti huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
Alhaj Mwinyi akatumia fursa hiyo kuwashukuru Viongozi, wanakijiji pamoja an waislamu wote waliochangia kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.
Nae, Mufti Mku wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab alisema ana imani kubwa kuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Dk. Hussein Mwinyi atafanikiwa kuwaunganisha Wazanzibar kama alivyofanikiwa Mtume Muhammad (SAW).
Aidha, kwa niaba ya wanakijiji wa Ghana Kichakani, Comodo Azana Hassan Msingiri aliishukuru Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja pamoja na ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kati Unguja kwa mashirikiano makubwa waliyotoa kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.
Alisema pamoja na msikiti huo kutumika kwa shughuli za ibada, lakini pia utakuwa chachu ya kubadili tabia za baadhi ya wanakiijiji wa maeneo hayo.
Mapema, Khatibu katika Sala hiyo ya Ijumaa, Ust. Rajab Abdillah Haji alitoa ahadi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinfduzi la kuutunza msikiti huo, sambamba na kuutumia kikmailifu kwa ajili ya kutoa elimu ya Dini kwa waumini wa maeneo hayo.