RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema waumini wa Dini ya kiislamu wana wajibu wa kuhakikisha Misikiti inatumika kwa ajili kufahamu mahitaji ya wananchi wa makundi tofauti waliopo katika maeneo husika na kuyatafutia ufumbuzi.Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya Ufunguzi wa Msikiti wa ‘Masjid Nuur Al-Rahman’ , uliopo Fuoni Kipungani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema katika maeneo ya Misikiti, kuna watu wa makundi tofauti, ikiwemo mayatima, wazee, walemavu na wengineo, hivyo ni wajibu wa waumini kuitumia mistikiti ili kufahamu mahitaji yao pamoja na kutafuta njia za kuwasaidia.“Sio vyema kwa msikiti kuishia katika suala la Ibada ya sala pekee, msikiti huu utumike kufahamu mahitaji ya wananchi wa makundi tofauti waliopo hapa na kuwasaidia”, alisema.
Aidha, Alhaj Mwinyi alieleza umuhimu kwa msikiti huo kutumika ipasavyo kwa ajili ya kuwaendeleza waumini kitaaluma na kubainisha uwepo wa mwamko mkubwa kwa vijana ambao walishiriki kikamilifu katika madrasa mbali mbali katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini hao kuwepo kwa matukio mbali mbali maovu yanayopaswa kushughulikiwa kupitia vikao vya msikiti huo, ikiwemo wizi na matumzii ya dawa za kulevya, kwa kuzingatia kuwa masuala hayo ni ya kijamii.Katika hatua nyengine, Alhaj Dk. Mwinyi alizitolea ufafanuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi hao, ikiwemo uwepo wa Barabara mbovu kutoka eneo la Ijitimai hadi Fuoni Kipungani.
Alisema Serikali itaishughulikia ujenzi wa barabara hiyo kupitia mradi wa ujenzi wa barabara za ndani, mbali na kuwa haikuwemo kabla kwenye orodha ya barabara hizo.Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa (Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa) kushughulikia changamoto ya kiusalama inayowakabili wananchi wa eneo hilo kwa kukaa pamoja na Uongozi wa Msikiti huo ili kufanikisha ujenzi wa kituo kidogo cha Polisi.
Alhaj Dk. Mwinyi aliwahakikishia waumini hao hatua thabiti zitakazochukuliwa na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ili kuondokana na changamoto ya umeme mdogo inayowakabili.Aidha, alimshukuru Mfadhili wa ujenzi wa msikiti huo, huku akiwataka waumini kumuombea dua, sambamba na kuliombea dua Taifa pamoja na yeye mwenyewe ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake ya kuliletea Taifa maendeleo.
Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saaleh Omar Kaab aliwataka waumini hao kuutunza vyema msikiti huo pamoja na kujenga mshikamano katika utekelezaji wa ibada, huku akisisitiza kumuombea dua mfadhili wa ujenzi wa msikiti huo.
Mapema, Katibu wa Muti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, akitoa salamu za Ofisi ya Mufti, alisema Ofisi hiyo imefurahi kutokana na ujenzi wa msikiti huo mkubwa, mzuri na wa kisasa.Sheikh Khalid alitoa wito wa kutumia vyema fursa kama hiyo pale inapotokea kwa kujenga misikiti ya kisasa na yenye kukidhi mahitaji ili waumini waweze kuswali katika mazingira bora.
Aidha, katika Risala ya Uongozi wa Msikiti huo, iliosomwa na Sheikh Mohamed Suleiman, ilisema pamoja na msikiti huo kuwa na jukumu la kuwaunganisha waumini kielimu, unakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya miundombinu mibovu ya barabara, umeme mdogo pamoja na usalama mdogo katika eneo la msikiti kutokana na kituo cha Polisi Fuoni kuwa masafa marefu.
Kwa upande wake, Khatibu katika Sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Othman Maalim aliwataka waislamu kuendeleza muamala wa Kiislamu kwa kuzingatia maisha ya jamii ya kila siku na kuondokana na dhana ya kuwa inatosha kwao kukamilisha nguzo za Dini ya Kiislamu pekee.“Uislamu ni uhalisia na maisha yaliokamilika na sio tu ndani ya msikiti…...Mtume Muhammad (SAW) alikuwa akiwajuilisha watu kwa wengine kutokana na tabia na mienendo yao”, alisema.
Alisema waislamu wamepigiwa mfano na Mtume Muhammad (SAW) kwa dhamira ya kuwafaa watu kutokana na amali na tabia zao njema.
Akinasibisha an kauli yake, Sheikh Othman alisema mtu aliejenga Msikiti huo amefanya jambo jema la kuwafaa watu wengine na kubainisha kuwa ‘amali nzuri ni lile jambo litakalofanywa na muumini na kuwatia furaha katika mioyo yao au kuwaondolea matatizo yanayowakabili’.
Wakati huo huo, kama ilivyo utaratibu wake, Alhaj Dk. Mwinyi alipata fursa ya kumtembelea na kumjuilia hali mzee Ali Rijali Mavua mwenye umri wa miaka 106, anaeishi katika eneo la Kwa Mchina.