Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha ahadi zilizoahidiwa kwa wananchi zinatekelezwa ipasavyo.

Alhaj Dk. Mwinyi ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Ijumaa Fumba Bondeni, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa anaamini kwamba bado changamoto za kimaendeleo zipo lakini juhudi zitaendedea kuchukuliwa usiku na mchana na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi aliwanasihi waumini wote nchini kuendelea kuomba dua ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu kuweza kutekeleza yale aliyoyaahidi.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi aliwaahidi waumini wa Msikiti huo wa Ijumaa Fumba Bondeni kuzipatia ufumbuzi changamoto zao zinazowakabili ambazo walizitoa mbele yake ikiwemo huduma ya maji safi na salama.

Nae Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume aliwasisitiza waumini wote nchini kuendelea kumuombea dua Rais Dk. Mwinyi ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani ana kazi kubwa ya kuwaongoza wananchi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo endelevu.

Sambamba na hayo, Sheikh Khalid aliwataka waumini kuhakikisha wanazitumia vyema ndimi zao kwani ni miongoni mwa viungo ambavyo kiongozi wa Waislamu Mtume Mohammad (S.A.W), amesisitiza vitumiwe vizuri ili kuepuka na adhabu za Mwenyezi Mungu huku akisisitiza kusema na kutenda yaliyomazuri.

Mapema akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Maulid Issa Shani aliwanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kuendelea kufanya mambo mema kwani kila analofanya mja ninajulikana na linaandikwa na hatimae atalipwa kwa jema ama ovu alilolifanya.

Pamoja na hayo, Sheikh Maulid Issa Shani katika hotuba yake hiyo alieleza kwamba Mwenyezi Mungu atawalipa waja wake kutokana na amali zao walizozifanya duniani hivyo, alisisitiza haja ya kuendelea kutenda mambo mema na kuepukana na kutenda maovu.