Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uongozi wa Masjid Kheir, Markaz ya Mombasa Zanzibar kwa kazi nzuri ya kutoa elimu ya dini kwa vijana.
Alhaj Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo wakati alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya Sala ya Ijumaa huko Masjid Kheir, Markaz iliyopo Mombasa, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika salamu zake hizo Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa mbali ya daawa inayotoa Markaz hiyo pia imekuwa ikitoa elimu kwa vijana jambo ambalo ni la kupongezwa kwani lina umuhimu mkubwa katika Uislamu.
Aliongeza kuwa katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan amekuwa akiungana na waumini katika misikiti mbali mbali kusali sala ya Taraweh na kuwaona jinsi vijana wanavyoosalisha na kusoma vyema Qur-an ambao wengi wao ni chimbuko la Markaz hizo.
Aidha, katika salamu hizo pia, Dk. Mwinyi alisisitiza juu ya suala zima la kuidumisha nchi katika amani pamoja na kumuomba MwenyeziMungu kuendelea kuipa neema.
Nae Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume alimueleza Alhaj Dk. Mwinyi kwamba Markaz hiyo imekuwa ikitoa vijana ambao leo hii wengi wao wamekuwa wakisalisha na kutoa elimu katika misikiti mbali mbali hapa nchini.
Mapema akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Ahmen Seif Nassor alieleza umuhimu wa funga ya Ramadhan pamoja na faida zake huku akisisitiza haja kwa waumini kutoa sadaka zao hasa katika kipindi hichi cha mwezi huu mkutufu kama ilivyosisitiza Qur-an pamoja na Mtume Muhammad (S.A.W).