Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasihi wafanyabiashara kuacha kuongeza bei ya vyakula hasa katika kipindi hichi cha kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Ijumaa Malindi, Mjini Zanzibar.
Katika salamu hizo Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba hivi karibuni kumekuwa na kupanda kwa bei ya bidhaa ikiwemo vyakula kwa kisingizio cha kupanda kwa gharama za usafiri na ununuzi ya bidhaa hizo huko nje kutokana na matatizo ya UVIKO -19.
Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba upo ukweli wa kupanda kwa bidhaa hizo lakini wafanyabiashara wengine wanatumia nafasi hiyo kupandisha zaidi licha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuchukua hatua ya kukaa na wafanyabiashara na kupunguza ushuru.
Aliongeza kuwa nia na madhumuni ya kufanya hivyo ni kuweza kuhakikisha bidhaa zinakuwa nafuu hivyo, aliwaeleza wafanyabiashara kwamba hatua hiyo imechukuliwa kwa madhumuni ya kuhakikisha unafuu wa biadhaa unapatikana na wananchi hususan wanyonge hawapati ugumu wa maisha katika kipindi cha kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Naomba nichukue fursa hii niwasihi wafanyabiashara wasije wakatumia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kupandisha bei bidhaa hususan vyakula”, alisema Alhaj Dk. Mwinyi.
Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Tume ya Ushindani Halali wa Biashara kuhakikisha unatumia sheria zilizokuwepo kuwadhibiti wale wote ambao nasaha hizo zinazotolewa na Serikali hawasizikilizi na badala yake wanaendelea kupandisha bei ya bidhaa kiholela.
Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba wafanyabiashara wengine watatumia fursa ya Serikali ya kupunguza ushuru ili na wao wapate kuongeza bei ya bidhaa jambo ambalo sio sahihi na kusisitiza kwamba hatua za kuwasihi zichukuliwe kwanza na watakapokaidi basi wachukuliwe hatua za kisheria.
Alhaj Dk. Mwinyi aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekubali kupata ushuru mdogo lakini inahakikisha wananchi wake wanapata unafuu wa bei za bidhaa hasa vyakula.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa waumini wa Msikiti huo kwa kumuita makusudi kwa azma ya kwenda kumuombea dua.
Akisoma hotuba ya sala ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti huo Sheikh Mohammed Mrisho Yussuf aliwataka Waislamu kufanya toba ya kweli na baada ya hapo kufanya mema na kutofanya kosa alilolifanya hapo siku za nyuma na kujuta.
Alisisitiza kwamba itakapofanywa toba ya kweli MwenyeziMungu hutoa msamaha wa makosa yaliyofanyika na kuwatia peponi waja wake waliotubia kikweli.
Pamoja na hayo, Sheikh Mohammed Mrisho Yussuf aliwasisitiza Waumini kufanya mambo mema hasa katika mwezi huu wa Shaaban ambao ni mwezi ambao Mtume Mohammad (S.A.W), alifanya mambo mengi mema ikiwemo kufunga, huku Masahaba na Waumini waliopita waliutumia vyema mwezi huu kuzidisha ibada na kuwasaidia wanyonge katika kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Mapema Alhaj Dk. Mwinyi alizuru makaburi ya Wazuoni waliozikwa katika eneo la msikiti huo na kuwaombea dua.