RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka waislamu kuendelea kukumbushana na kuwahamasisha watu wenye uwezo; kutoa sadaka zao kwa watu wenye uwezo duni.
Alhaj Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika salamu zake kwa waislamu walioshiriki katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, iliofanyika katika Msikiti Mweupe Chaani Kubwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza na waumini hao, Alhaj Mwinyi alisema kwa niaba yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, anatoa shukurani kwa wananchi wote wa Zanzibar waliotoa misaada mbali mbali kwa waislamu wenye uwezo mdogo katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, wakiwemo Sheikh Ariff na Sheikh Rashid Mazrui kutoka taasisi ya Miraj Tanzania ambao walishiriki katika ibada hiyo.
Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani za dhati kwa wananchi wa Sehiya ya Chaani kubwa kutokana na dua waliyomuombea ili aweze kuwa na afya njema na kutekeleza vyema majukumu yake ya kitaifa.
Alitumia fursa hiyo kumuomba Mwenyezi Mungu kutakabal funga za waja wake.
Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume, aliwataka wananchi wa shehiya ya Chaani Kubwa kuendelea kumuombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Mwinyi, ili aweze kiutekeleza vyema majukumu yake akiwa mwenye afya njema.
Sheikh Arrif kutoka taasisi ya Miraj Tanzania aliwaomba wananchi wa Shehiya ya Chaani Kubwa na Zanzibar kwa ujumla, kumuombea Dua Alhaj Dk. Mwinyi ili aweze kuwatumikia waislamu na wananchi wote wa Zanzibar.
Mapema, Khatibu katikasala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Abdulghafour Abdulrahim aliwakumbusha waislamu umuhimu wa kuendelea kutekeleza vyema ibada katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kama alivyofanya Mtume Muhammad (SAW), sambamba na kusafisha nyoyo zao.
Alisema saumu ni darasa linalowafunza waislamu , ambapo miongoni mwa mafunzo yaliomo ni usiku wa Lailat Qadr.
Katika ibada hiyo ya sala ya Ijumaa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alikabidhi sadaka kwa waislamu walioshirki katika ibada hiyo