RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kushindana katika kufanya mambo ya kheri, ikiwemo ujenzi wa misikiti.Alhaj Dk. mwinyi amesema hayo Kiboje Mkoa Kusini Unguja, wakati alipofungua Msikiti wa Ijumaa wa Al - Mubarak, hafla iliokwenda sambamba na Ibada ya sala ya Ijumaa msikitini hapo.

Amesema hatua inayoendelea kuchukuliwa na waumini na kujenga misikiti mizuri na ya kisasa katika maeneo mbali mbali ya nchi, ni jambo kubwa na la kheri linalofaaa kuendelezwa na waumini kwa kuzingatia fadhila kubwa zinazopatikana kutoka kwa Mwenyezi Mungu.Alisema ujenzi wa misikiti una njia nyingi, hivyo akawataka waumini wasio na uwezo kushiriki kwa namna yoyote ile, ili nao waungane na wafadhili katika kupata fadhila hizo.

Aidha, alisema kuna umuhimu kwa waislamu mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa misikiti hiyo kushiriki kikamilifu katika Ibada za sala, hususan za jamaa pamoja na kudumisha umoja miongoni mwao.Alhaj Mwinyi alisisitiza haja ya Misikiti kutumika katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili jami kupitia makundi mbali mbali kama vile wajane, walemavu, yatima na wagonjwa.

“Misikiti ina kazi nyingi za kheri, mbali na kutumika kwa ajili ya kufanya ibada ibada pia inapaswa kutumika katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii”, alisema.Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kuitunza an kuifanyia matengenezo misikiti ili iweze kuendeleea kubaki katika haiba yake na kudumu kwa kipindi kirefu.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Mfadhili pamoja na waumini wote waliofanikisha kukamilika kwa ujenzi wa msikiti huo.

Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab alisisitiza umuhimu wa waislamu kuendeleza umoja miongoni mwao na kuwataka kuutumia vizuri msikiti huo, huku akiomba baraka nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ziushukie msikiti nuo.Aidha, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume alitumia fursa hiyo kuwapongeza wale wanaofanya juhudi kwanamna tofauti ya kujenga misikiti kwa kigezo cha kupata fadhili nyungi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mapema, katika Risala yao, kwa niaba ya waislamu wa msikiti huyo iliosomwa na Ustadhi Ali Hassan Abdalla alisema, msikiti huo umejengwa chini ya Ufadhili wa Sheikh Ahmeid Nassor Al- Riami, ambapo umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 200 hadi kukamilika kwake, ukiwa na uwezo wa kuswaliwa na waumini 400 kwa wakati mmoja.Alisema pamoja na mambo mengine, mfadhili huyo analenga kujenga Madrasa, maduka, ofisi pamoja na nyumba kwa ajili ya Mwalimu wa Madrasa katika eneo hilo la Msikiti.