RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka waumini wa Dini ya kiislamu nchini kujipamba kwa tabia njema ili kupata fursa ya kuwa karibu na Mtume Muhammad (SAW) peponi.Alhaj Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo Mkwajuni Kidombo Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika nasaha zake kwa waumini walioshiriki Ibada ya Sala ya Ijumaa, iliokwenda sambamba na kisomo maalum (khitma) kwa wazee wa Kijiji hicho pamoja na maadhimisho ya uzawa wa Mtume Muhammad (saw) ambayo hufanyika kila mwaka.

Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa waumini wa Dini ya Kiislamu kujipamba kwa tabia njema pamoja na kuwafunza watoto wao umuhimu wa jambo hilo ili kupata fursa ya kuwa karibu na Mtume Muhammad (SAW) peponi.“Ili na sisi tuongoke na kulipwa mema tuna wajibu wa kujipamba kwa tabia njema ili tuweze kuwa karibu na Mtume Muhammad (SAW) peponi”, alisema.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mstaafu wa Zanzibar (awamu ya tano) Alhaj Dk. Salmin Amour Juma kwa mwaliko anaotowa kila mwaka, ambapo waumini kutoka maeneo mbali mbali nchini hupata fursa ya kushiriki katika maadhimisho hayo, huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumjaalia kila la kheir na afya njema.

Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, aliwataka waislamu kuendeleza tabia njema ya Mtume Muhammad (SAW) katika maisha yao, akibainisha kuwa ni kielelezo chema kwa binadamu wote.Alieleza kuwa Mtume Muhammad (SAW) alikuwa rehma hata kwa wanyama, na kusema hatua hiyo inaendana na ile ya Viongozi wa Taifa hili kwa kuwa na huruma na wananchi wao.

Mapema, Khatibu katika sala hiyo ya Ijumaa alisema Mtume Muhammad alikuwa rehma ambapo kutokana na tabia yake njema watu mbambali waliweza kusilimu.Katika hafla hiyo Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishirki, akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Alhaj Othman Masoud Othman, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa pamoja na Viongozi mbali mbali